2435; Kukusanya na kutawanya…
Kitu kimoja ambacho nazidi kujifunza kwenye eneo la mafanikio ni wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wanaanza na rasilimali zinazolingana.
Mwanzoni watu hao hawatofautiani sana kwenye eneo la rasilimali.
Kama ni muda wanakuwa nao sawa.
Akili pia hawatofautiani sana.
Na hata kwenye fedha, wengi huanzia chini wakiwa hawana fedha kabisa.
Lakini kadiri muda unavyokwenda, tofauti kubwa inaanza kuonekana baina ya wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa wanazidi kuwa na rasilimali nyingi kadiri wanavyokwenda.
Huku wanaoshindwa wakizidi kuwa na uhaba wa rasilimali.
Tofauti hiyo inatokana na mtazamo walionao watu hao.
Wanaofanikiwa huwa wana mtazamo wa kukusanya.
Rasilimali kidogo walizonazo wanazikusanya vizuri na kuweza kuzitumia kwa tija zaidi.
Kama ni muda wanautumia kwa mambo yenye tija pekee.
Kama ni fedha, hata kama ni kidogo kiasi gani, wanazikusanya na kuweza kuzitumia kwa njia ya kuzalisha fedha zaidi.
Na hata kwa akili zao na nguvu zao, wanazikusanya maeneo machache yenye tija na hivyo kuzalisha matokeo bora zaidi.
Wanaoshindwa huwa wana mtazamo wa kutawanya.
Rasilimali kidogo wanazokuwa nazo wanazitawanya hovyo, mwisho wake zinakuwa hazina tija wala manufaa kwao.
Muda wao wanautumia kwenye mambo yasiyokuwa na tija yoyote.
Fedha kidogo wanayokuwa nayo wanaidharau na kuutawanya hovyo, kitu kinachowatenganisha na kila fedha wanayokuwa nayo.
Hata akili, nguvu na umakini wao, wanavitawanya kwenye mambo mengi kiasi kwamba hakuna lolote linalofanyika kwa namna bora na ya kipekee.
Hebu yaangalie maisha yako huko ulikotoka mpaka hapo ulipofika sasa, tabia zako zimekuwa za kukusanya au kutawanya?
Jitathmini kwa rasilimali ndogo ndogo unazokuwa nazo, iwe ni fedha kidogo unazopata na hazina mpangilio au muda mfupi unaopata na huna cha kufanya.
Je huwa unakusanya au kutawanya?
Pata majibu sahihi kisha chukua hatua sahihi.
Kila siku jikumbushe kukusanya na siyo kutawanya.
Kocha.