2436; Kuiga mpaka uwe…

Huwa kuna kauli maarufu ya Kiingereza inayosema; fake it till you make it.
Ikiwa inamaanisha chochote kile unachotaka, unapaswa kukiigiza mpaka kiwe kweli kwenye maisha yako.

Na dhana kuu ni kwamba akili yetu ya ndani huwa haiwezi kutofautisha ukweli na maigizo. Yenyewe inachukulia kile mtu anachofanya kama ni sehemu ya maisha yake na hivyo kumpa fursa zaidi zinazoendana na kile anachofanya.

Watu wengi wamekuwa wanaielewa kauli hii vibaya, kwa kuigiza upande usio sahihi wa mafanikio.
Wengi wamekuwa wanaigiza upande wa mwonekano na matumizi, badala ya kuigiza upande wa kazi na misingi ya kuishi.

Kama unataka kuwa bilionea, usiigize matumizi ya mabilionea, badala yake igiza misingi yao ya maisha, ufanyaji wao wa kazi na mitazamo waliyonayo.

Kwa kuyaangalia maisha ya mabilionea utajionea wazi kabisa ni watu wanaojali sana mambo yao na kutokuhangaika na mambo ya wengine.
Watu wanaothamini sana muda wao na kuhakikisha hawapotezi hata sekunde moja.
Na ni watu wenye ndoto kubwa, wanaoziamini hasa na hawakubali kutetereshwa na chochote.
Na zaidi, ndoto zao ndiyo kipaumbele cha kwanza kwao, hawafanyi kila linalowezekana, bali wanafanya kila linalopaswa kufanyika.

Sasa wewe hebu iga huo upande tu na ishi kama ni kweli kwenye maisha yako.
Anza na ndoto kubwa na unazoziamini kabisa pasi na shaka yoyote ile.
Zipe ndoto hizo kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako.
Usijali wengine wanakuchukuliaje au wanafanya nini, wewe pambana na ndoto zako.
Na usipoteze muda wako kwa jambo lolote nje ya ndoto zako, wekeza muda wako, nguvu zako na umakini wako kwenye ndoto ulizonazo.

Iga hayo na yafanye kuwa sehemu ya maisha yako na utashangaa jinsi mambo mengi mazuri yatakuja kwenye maisha yako.

Hatua ya kuchukua leo;
Chagua kuiishi siku ya leo kama bilionea, siyo kwa upande wa matumizi, bali kwa upande wa nidhamu ya kazi na mtazamo.
Anza kwa kuipangilia siku yako nzima, usiwe na muda ambao huna cha kufanya.
Kila unachofanya kifanye kwa viwango vya juu sana, usifanye chochote hovyo hovyo.
Na kabla hujafanya chochote, jiulize je mabilionea huwa wanafanya hivyo?
Igiza siku hii moja kama bilionea na utaona jinsi inakwenda kuwa bora kwako.

Neno la kutafakari leo;
Iga kazi, iga mtazamo na iga misingi. Usiige matumizi.

Kocha.