2441; Kukata tamaa…
Kila mmoja wetu huwa anakutana na hali ya kukata tamaa katiks nyakati tofauti tofauti za maisha yake kulingana na kile anachokuwa anapitia.
Hali hii ya kukata tamaa haisababishwi na kile ambacho mtu unapitia, bali inasababishwa na namna mtu unatafsiri kile unachopitia.
Kuna mtazamo unaokuwa nao kuhusu unachopitia, mtazamo huo unachochea aina fulani ya fikra ambazo ndiyo zinaibua hisia unazokuwa nazo ambazo ni kukata tamaa.
Hiyo ina maana kwamba unachohitaji ili kuondokana na hali ya kukata tamaa siyo kubadilika kwa kile unachopitia, bali kubadili namna unavyokitafsiri.
Kubadili mtazamo ulionao juu ya kitu hicho, kitu kitakachobadili fikra unazokuwa nazo na hatimaye hisia zinabadilika.
Mfano pale unapokutana na magumu au mambo kwenda tofauti na ulivyopanga, badala ya kuchukulia huo ndiyo mwisho na anguko, chukulia ni maandalizi ya wewe kuwa bora zaidi.
Usione magumu unayopitia kama adhabu au anguko, bali yaone kama mafunzo ya kukuandaa kufanya na kupata makubwa zaidi.
Kwa kuanza na mtazamo huo, unakuwa na fikra za kutaka kujifunza zaidi ili uwe bora. Hilo linaleta hisia za shauku na matumaini, unaona namna unakwenda kuwa bora zaidi kwa yale unayofanya.
Hisia hizo zinakusukuma kukabiliana na chochote kile bila kukata tamaa na kukuwezesha kukivuka ukiwa bora zaidi.
Dunia haitabadilika ili kuendana na tunavyotaka sisi, bali tunapaswa kubadilika ili kuendana na inavyotaka dunia.
Ni rahisi kukata tamaa pale unapotaka dunia iende unavyotaka wewe, kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako kabisa.
Utaondokana na kukata tamaa pale unapoiacha dunia iende inavyoenda na wewe kubadili mtazamo wako kwenye yale unayopitia.
Hatua ya kuchukua;
Pale unapojikuta kwenye hali ya kukata tamaa, jiulize ni kwa namna gani unalazimisha dunia iende kama unavyotaka wewe.
Badili huo mtazamo, acha kutaka dunia iende unavyotaka na ipokee jinsi inavyoenda na uwe na njia bora ya kunufaika na vile dunia inavyoenda.
Tafakari;
Umezaliwa ukaikuta dunia na utakufa uiache. Huna mamlaka ya kuipangia dunia iendeje. Hivyo acha kujihangaisha na hilo, wewe endana na vile dunia inavyokwenda na hutajikuta kwenye hali ya kukata tamaa.
Kocha.
Nashukuru Sana kocha makala hii yenye tafakari, na hatua ya kuchukua.
LikeLike
Karibu
LikeLike