2443; Unahitaji kufikiri kwa utofauti.
Albert Einstein aliwahi kunukuliwa akisema ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile halafu kutegemea kupata matokeo ya tofauti.
Unaweza kuona hii ni kauli ambayo haikuhusu, lakini hebu itafakari kwa kina.
Kuna maeneo ya maisha yako ambayo umekuwa unapata matokeo yale yale, japo ni matokeo ambayo huridhiki nayo.
Inaweza kuwa ni kwenye upande wa kipato, ambapo kipato chako kimegota kwenye kiwango fulani kwa muda mrefu.
Inaweza kuwa pia kwenye biashara ambapo wateja wamekuwa ni wale wale kila siku.
Kabla hujalalamikia matokeo unayopata kwenye maisha yako, hebu angalia kwanza juhudi unazoweka.
Kama juhudi ni zile zile, unategemeaje upate matokeo ya tofauti?
Unahitaji kufanya kwa utofauti ili uweze kupata matokeo ya tofauti kabisa.
Na ili ufanye kwa tofauti, unapaswa kuanza kufikiri kwa tofauti kabisa.
Fikiri kwa namna ambayo hujawahi kufikiri.
Fikiri bila ya kujiwekea ukomo au kujikatisha tamaa.
Kisha njoo na njia tofauti za kufanya kile unachofanya.
Kwa njia hiyo utaweza kuzalisha matokeo ya tofauti na kupiga hatua kubwa.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila eneo la maisha yako ambalo unaona umefika ukomo, kaa chini na jiulize ni namna gani unawesa kufanya kwa tofauti. Orodhesha majibu yasiyopungua 20 ya namna unaweza kufanya kwa tofauti. Usidharau jibu lolote au kujiambia haliwezekani.
Wewe orodhesha majibu kwanza kisha baadaye utachagua machache uyakayoanza kufanyia kazi.
Kwa njia hiyo utaweza kupata matokeo ya tofauti na unayopata sasa.
Tafakari;
Eneo lolote ambalo unaona umefika kwenye ukomo, huo siyo mwisho wa eneo hilo, bali ni mwisho wa kufikiri kwako kwa sasa. Kama unataka kwenda zaidi ya hapo, lazima ufikiri kwa utofauti kabisa.
Kocha.