2445; Kuwa tayari kukosea.

Kama kuna kitu kimoja muhimu sana cha kujifunza kutoka kwenye mfumo wa elimu ni hiki; mafanikio siyo kutokukosea kabisa.

Kwenye mfumo wa elimu mafanikio hupimwa kwa ufaulu wa mitihani.
Lakini haimaanishi unapaswa kupata alama 100 ndiyo uwe umefaulu.

Hata daraja A ambalo ni la juu kabisa, linaanzia alama 75. Hiyo ina maana hata kama utakosa robo ya maswali yote, bado una ufaulu wa juu kabisa.

Na kingine zaidi ni hata kama utakosa nusu ya maswali yote, bado utakuwa umepata daraja la ufaulu. Yaani ukipaga alama 50 kati ya 100, umefaulu.

Tunajifunza nini kwenye mafanikio?
Kwamba huhitaji kupatia mara zote ndiyo ufanikiwe.
Unaweza kukosea mara nyingi na bado ukafanikiwa.
Kuliweka vizuri hilo, bila kukosea hakuna mafanikio.

Hivyo tunapaswa kuwa tayari kukosea, tunapaswa kuwa tayari kushindwa kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kupata mafanikio kwenye maisha.

Kukosea na kushindwa maana yake ni umejaribu vitu vipya na vikubwa kuliko ulivyozoea.
Japokuwa utashindwa kwenye baadhi, utaondoka na funzo kubwa sana.
Na bado utakuwa kwenye nafasi ya kufanikiwa kwenye baadhi ya vitu hivyo.

Ondokana na hofu ya kushindwa ambayo ndiyo inakuzuia usifanye mambo mapya na makubwa.
Hakuna mafanikio kama hujafanya mapya na makubwa.
Na hayo mapya na makubwa yana hatari ya kukosea na kushindwa.
Lakini hiyo haimaanishi ndiyo mwisho, bali ni hatua nzuri ya kuweza kufanikiwa zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Angalia ni makosa gani ambayo umekuwa unahofia kuyafanya kwenye safari yako ya mafanikio na jua hicho ndiyo kikwazo cha mafanikio yako.
Kuanzia sasa kuwa tayari kukosea ukijua ndiyo njia ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.
Jaribu mambo mapya na makubwa kuliko ulivyozoea na utajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi.

Tafakari;
Kama hukosei, maana yake hakuna mapya na makubwa unayofanya.
Na hilo litakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.
Jenga hamu yako ya kushindwa ili uwe kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.

Kocha.