2448; Ukiwa njia panda, chagua kazi zaidi…
Pale unapojikuta njia panda, ukiwa hujui uchague kipi kati ya vingi vilivyo mbele yako, mara zote chagua kile kinachotaka kazi zaidi.
Najua hili ni kinyume na wengi tunavyofikiri na kuamua.
Huwa tunakimbilia kuchagua kile ambacho ni rahisi na hakihitaji kazi zaidi.
Na hiyo ni moja ya kikwazo cha mafanikio makubwa.
Kuna sababu tatu za kuchagua kazi zaidi.
Moja ni kazi ndiye rafiki wa kweli, ambaye hawezi kukutupa wala kukuonea wivu. Ni rafiki ambaye ukimjali naye anakujali.
Mbili ni watu wengi huwa hawapendi kazi na hivyo kuikimbia. Hilo linaacha fursa kubwa kwenye maeneo yanayohitaji kazi zaidi, kwani hayawi na watu wengi wanaoyakimbilia. Panapohitaji kazi zaidi hakuna ushindani mkubwa.
Tatu ni hakuna kazi inayokwenda bure, kazi yoyote ya ziada unayofanya, asili itahakikisha unalipwa kwa ziada pia. Hivyo unavyofanya kazi zaidi, ndivyo pia unavyolipwa zaidi.
Usiwe kama wengi ambao wanakimbilia urahisi, wewe kimbilia kwenye kazi zaidi na manufaa yake utayaona.
Hatua ya kuchukua;
Tumia kigezo cha kazi na ugumu kwenye kufanya maamuzi yako yote ya nini ufanye. Kila unapojikuta njia panda, ukiwa na machaguo mengi na hujui uchague nini hasa, wewe angalia lile chaguo gumu zaidi au linalotaka mtu ufanye kazi zaidi na nenda na hilo.
Wachache sana ndiyo watakaochagua hilo na chochote cha ziada utakachofanya kitakulipa kwa ziada pia.
Tafakari;
Watu wengi huwa wanapenda kufanya vitu rahisi ndiyo maana hawafanikiwi, maana kwenye urahisi ushindani ni mkubwa. Wachache wanaofanikiwa ni wale walio tayari kufanya vitu vigumu, hivyo havina ushindani na hata thamani yake ni kubwa pia.
Je wewe unachagua nini? Rahisi au kazi?
Kocha.
Asante Sana kocha Dr. Makirita Amani, nachagua kazi zaidi kwa chochote ninachofanya
LikeLike
Safi sana.
LikeLike
Vizuri.
LikeLike