2449; Kila kitu ni fursa.

Umewahi kushangaa unapita mahali kila siku na huoni kitu cha tofauti, ila anakuja mtu mwingine na kuona fursa kubwa na anayoitumia kunufaika sana?

Umewahi kushangaa unafanya kazi au biashara kwa muda mrefu, ila anakuja mtu mwingine na kuifanya kwa ubora wa kipekee sana kitu kinachompa manufaa makubwa?

Hatua ya kwanza ya kuziona fursa ni kuzitafuta.
Huwezi kupata kitu kama hukitafuti.
Na inapokuja kwenye fursa, wanaoziona ni wale ambao wanazitafuta wakati wote.

Upo msingi mmoja ambao ukiuishi kila siku utaweza kuziona fursa nyingi sana kwenye maisha yako.

Msingi huo ni kila kitu ni fursa.
Ianze kila siku yako kwa msimamo huo, kwamba kila kinachotokea na unachokutana nacho kwenye siku yako ni fursa.

Na hapa namaanisha kila kitu.

Iwe ni mahali umechelewa itumia hiyo kama fursa ya kujua namna unaweka vipaumbele vyako.

Iwe ni mtu amekukwaza na kukuudhi itumie kama fursa ya kudhibiti hisia zako.

Iwe ni mtu ulimtegemea akakuangusha tumia kama fursa ya kujua watu sahihi wa kushirikiana nao.

Iwe ni watu wamekuchelewesha mahali au umekutana na foleni tumia kama fursa ya kujifunza.

Iwe ni kipato chako hakitoshelezi, itumie kama fursa ya kupata njia zaidi za kuingiza kipato.

Ukikuta watu wanalalamika au kulaumu jiulize kuna fursa gani hapo ambayo unaweza kuifanyia kazi.

Ukikutana na kitu ambacho watu wanakikimbia kwa sababu ni kigumu, wewe angalia ni fursa gani kubwa iliyo ndani ya kitu hicho.

Kila kitu kipya unachojifunza, angalia ni namna gani unaweza kukifanyia kazi kwenye maisha yako na hapo utazifungua fursa mbalimbali.

Fursa zipo wazi kwa watu wote, ila wanaoziona ni wale wanaozitafuta.
Kuwa mmoja wa hao wanaotafuta fursa na utaweza kunufaika sana.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila siku yako, chukulia kila kitu kama fursa. Kwa kila unachopitia au kukutana nacho, jiulize hapa kuna fursa gani? Kisha ona kitu cha tofauti unachoweza kufanyia kazi.
Hata kama ni kidogo kiasi gani, wewe fanyia kazi na hatua hizo ndogo ndogo zitakuja kuzaa matunda makubwa sana.

Tafakari;
Kabla hujahangaika kwenda mbali kutafuta fursa, hebu anzia hapo hapo ulipo sasa. Kabla hujatafuta kazi nyingine, hebu angalia kama umeshatumia fursa zote zilizo kwenye kazi unayofanya sasa.
Kabla hujaenda kuanzisha biashara nyingine, hebu angalia kama umeshatumia kila fursa iliyopo kwenye biashara unayofanya sasa.
Fursa huwa ni nyingi kila mahali, lakini hatuzioni kwa sababu hatuzitafuti.
Wewe kuwa wa tofauti kwa kuchukulia kila kitu kama fursa na hilo litakuwezesha kuziona fursa nyingi.

Kocha.