2450; Hakuna Aliyekamilika.

Sisi binadamu tuna changamoto na mapungufu mbalimbali.
Hivyo ndivyo asili yetu ilivyo.

Kama ilivyo kwamba ndege ni usafiri mzuri na wa haraka, ila ajali yake ni hatari kubwa sana.

Inawezekana kabisa kutengeneza ndege ambayo ni salama kwenye ajali, lakini haitaweza kuruka hewani.

Ni kanuni ya asili kwamba kupata kimoja lazima iwe tayari kupoteza kingine (trade-offs).

Mahusiano mengi baina ya watu yamekuwa na changamoto kubwa kwa sababu kila mtu anataka mwenzake awe mkamilifu, awe vile anavyotaka yeye awe.

Hapo ni sawa na kutaka samaki aweze kuishi kwenye maji, nchi kavu na aruke angani.
Hilo haliwezekani kabisa.
Kinachomfanya samaki aweze kuishi kwenye maji, ndiyo kinachokuwa kikwazo kwake kuweza kuishi nchi kavu.

Hakuna aliyekamilika, bali kila mtu ana umuhimu wake.
Kila mtu kuna kitu anaweza kukifanya vizuri kuliko wengine na kikawa na manufaa makubwa kwa wote.

Hivyo unapojenga mahusiano yako na watu wengine, usiangalie sana wamekosa nini au madhaifu yao ni yapi, bali angalia nini cha kipekee walichonacho na jinsi kilivyo na manufaa kwako.

Unapoangalia matatizo au changamoto za watu, utaona hizo kwa wingi. Kitu kitakachokukatisha tamaa na uone hakuna watu sahihi.

Ukiangalia upekee au uimara wa watu, utaona hayo, kitu kitakachokufanya uone umuhimu wao na mshirikiane vizuri.

Hii haimaanishi kila mtu ni sahihi kwako, bali unapaswa kuchagua wale ambao wanakitu kinachoweza kuwaweka pamoja.

Na wala haimaanishi uvumilie kila uzembe ambao watu wanao. Lazima ujiwekee viwango vya watu unaoshirikiana na kuhusiana nao.

Kuna tabia ambazo ni mbaya na watu wanazo, hizo hazihusiani kabisa na madhaifu yao ya asili.
Tabia kama uongo, wizi, uvivu, kukosa uaminifu ni tabia ambazo hata kama mtu anazo, anapaswa kuonyesha juhudi za kuachana nazo.

Katika ushirikiano na mahusiano yako na wengine, tambua hili muhimu, huendi kukutana na mtu ambaye amekamilika kila idara.
Bali unakutana na mtu ambaye ana uimara kwenye maeneo fulani, udhaifu maeneo mengine na anayepambana kuwa bora zaidi kila siku.

Hatua ya kuchukua leo;
Tafakari mahusiano yote bora uliyonayo, utaona wazi kuna vitu vya muhimu unapata kwa watu hao, licha ya kwamba kuna madhaifu waliyonayo.
Pia tafakari mahusiano mabovu uliyonayo au umewahi kuwa nayo, utaona ulitegemea mtu awe amekamilika au uimara wake haukuwa muhimu kwako.
Boresha kila mahusiano uliyonayo kwa kuangalia manufaa gani unayopata kwa mtu na komaa zaidi na hayo badala ya madhaifu anayokuwa nayo.

Tafakari;
Ni vigumu sana kukuta sifa zote unazozitaka kwa mtu mmoja. Jenga mahusiano yako na wengine kwa kuangalia uimara ambao tayari wanao na ambao unahitaji na siyo kujifanganya unakwenda kuwabadili wawe kama unavyotaka wewe.
Ukipata ambao tayari wanapambana kuwa bora kutoka ndani yao, una bahati zaidi.

Kocha.