2452; Usijumuishe.
Kufanya maamuzi ni kugumu kwa sababu kuna mambo mengi ambayo tunakuwa hatuyajui juu ya kile tunachotaka kuamua.
Kuepuka ugumu huo huwa tuna tabia ya kutafuta njia ya mkato ya kutuwezesha kufanya maamuzi.
Na moja ya njia hizo ni kujumuisha.
Kwa njia hii, vitu vyote vyenye sifa moja unavijumuisha pamoja.
Hivyo unafanya maamuzi kwa kundi zima na siyo kwa kitu kimoja kimoja.
Kwa mfano kama wa kabila fulani amekukwamisha basi unachukulia watu wote wa kabisa hilo ni wa kwamishaji.
Au kama mtu wa rangi au jinsia fulani amekusumbua basi unachukulia wengine wote wenye sifa kama zake nao ni wasumbufu.
Japo njia hii itakuwezesha kufanya maamuzi haraka, lakini siyo maamuzi bora na sahihi.
Ni maamuzi ambayo yanakuwa na makosa mengi sana.
Japokuwa watu kwenye kundi moja wanaweza kufanana baadhi ya sifa, bado kufanya maamuzi wanafanya kama mtu mmoja na siyo kundi.
Wengi hufanya maamuzi kulingana na kile wanachojua na hisia wanazokuwa nazo pia.
Na kwa kuwa hisia za wengi hubadilika mara kwa mara, hata maamuzi yao hubadilika pia mara kwa mara.
Hivyo unapofanya maamuzi, usijumuishe watu au vitu vyote kwenye kundi moja kwa kutumia uzoefu wako wa nyuma.
Badala yake fanya maamuzi kwa kuangalia kitu au mtu kwa upekee wake.
Hilo litafanya maamuzi kuwa magumu, ila yatakuwa maamuzi bora kabisa.
Hatua ya kuchukua;
Usiwaadhibu watu wote kwa kosa la mtu mmoja. Mteja mmoja ametumia biashara yako isivyo sahihi usikimbilie kuweka sheria ambayo inawanyima wateja wengine uhuru wa kuitumia ilivyo sahihi.
Mfanyakazi wako mmoja ametumia vibaya rasilimali usiweke sheria inayowazuia mpaka wale wanaozitumia vizuri.
Fanya maamuzi kwa mtu mmoja mmoja na siyo kwa kujumuisha wote.
Kila unapojikuta unajumuisha katika kufanya maamuzi, jikumbushe haupo sahihi, kuna wengi ambao wanafanya tofauti na majumuisho yako.
Tafakari;
Chochote rahisi kufanya huwa hakina thamani kubwa, kwa sababu kila mtu anaweza kufanya.
Thamani kubwa ipo kwenye vitu vigumu kufanya, ambavyo wachache pekee ndiyo wanaofanya.
Moja ya vitu hivyo ni kufanya maamuzi kwa binafsi badala ya kujumuisha.
Utahitaji taarifa nyingi na utulivu mkubwa, lakini yatakuwa maarifa bora kabisa.
Kocha.