2453; Ukiwa huna cha kupoteza.

Umewahi kugundua kwamba ukiwa na fedha huwa hazikosi matumizi?
Na ukiwa huna fedha bado maisha hayasimami?

Yaani ukiwa na fedha, utashangaa zinatumika na bado yale mahitaji muhimu uliyonayo yanakuwa hayajaisha.

Kadhalika ukiwa huna fedha, hata kama una mahitaji mengi kiasi gani ambayo hujaweza kuyatimiza, bado maisha yataendelea.

Kadhalika kwenye muda, siku ambayo huna muda kabisa, yaani siku ambayo umebanwa sana ndiyo siku unayokamilisha mengi zaidi.

Lakini siku ambayo unajiambia una muda wa kutosha ndiyo siku ambayo hakuna makubwa unafanya.
Unaimaliza siku ukiwa umechoka lakini ukiangalia hakuna ulichokamilisha.

Kwa asili, sisi binadamu tunapokuwa na kitu kwa wingi, huwa tunatafuta njia ya kukipoteza.
Inatokea tu tunajikuta tukitumia vibaya kile ambacho tunacho kwa wingi.

Lakini tusipokuwa na kitu kwa wingi, tunakuwa hatuna cha kupoteza, na hivyo hatupotezi.
Tunapokuwa na uhaba wa kitu, tunakithamini kweli na kuhakikisha hakipotei.
Tukiwa na wingi wa kitu, tunajisahau na kuanza kukipoteza.

Ukiwa na fedha ambayo hujaipangilia na ukakutana na kitu kinauzwa, ni rahisi kushawishika kununua.
Ukiwa huna fedha, huwezi kununua kitu hicho.

Ukiwa una muda mwingi ambao huna cha kufanya na ukasikia kuna habari fulani zinaendelea utazifuatilia.
Ukiwa umetingwa na huna muda kabisa, hutahangaika na habari hizo.

Tunapokuwa na vitu vya kupoteza, hilo ndiyo linalotokea, tunavipoteza.
Lakini tunapokuwa hatuna cha kupoteza, hatupotezi chochote.

Hatua ya kuchukua;
Jiweke kwenye hali ambayo huna cha kupoteza.
Kwa upande wa fedha hakikisha kila fedha uliyonayo umeipangia matumizi na kama haina matumizi basi iweke mahali ambapo haitakuwa rahisi kuitoa.
Kwa upande wa muda hakikisha muda wako wote umeupangilia utafanya nini, ili usiwe tu na muda ambao huna cha kufanya.
Epuka sana kuwa na chochote cha ziada ambacho hakijapangiliwa, kwani utaishia kukipoteza.

Tafakari;
Kuanza biashara kwa mtaji kidogo au bila mtaji ni faida kubwa, maana hutakuwa na fedha za kupoteza. Utahangaika na yale muhimu tu na akili yako itatulia kwenye biashara na siyo kwenye mambo yasiyo na umuhimu.
Kama unakosa utulivu kwenye kile unachofanya, sababu kubwa inaweza kuwa una vingi vya kupoteza na hivyo unavipoteza.
Dhibiti vitu hivyo ili usiwe na cha kupoteza.

Kocha.