2456; Kujaribu.
Mbwa huwa hajaribu kubwa mbwa, bali anakuwa mbwa.
Kadhalika ukipanda mahindi, mche unapoota haujaribu kuwa mhindi, bali unakuwa.
Kila kitu kwenye asili tayari kina uwezo na upekee ndani yake.
Kinachopaswa kufanya siyo kujaribu bali kuwa.
Hakipaswi kuiga vitu vingine bali kinapaswa kuwa kilivyo.
Lakini inapokuja kwetu binadamu, pamoja na uweze mkubwa wa akili zetu, tumekuwa tunazitumia vibaya.
Tunahangaika kujaribu mengi yasiyotufaa, wakati ndani yetu tayari tunacho kile cha kutufaa.
Ukishajiona unahangaika na kujaribu mambo mengi, jua umechagua kujisahau wewe mwenyewe na kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwako.
Ukiona unajiambia unajaribu kitu fulani, jua kabisa hicho siyo sahihi kwako, hivyo kuna uwezekano utapoteza tu muda kwenye hilo.
Kwenye asili hakuna kujaribu, kuna kuwa au kutokuwa.
Simba anapomuona swala hasemi anajaribu kumkamata ili apate chakula, bali anajiambia hiki ndiyo chakula na kuweka kila kitu chake hapo.
Kadhalika swala anapomuona simba, hajiambii anajaribu kukimbia, bali anajua hilo ni swala la kufa na kupona, akimbie apone au azembee afe.
Asili haina huruma, haiangalii nani anataka sana au anajaribu. Inatoa kile kinachopaswa kulinga na namna kitu kimejitoa ili kupata.
Hivyo kama unataka kitu, usiige wala usijaribu, kuwa vile ambavyo tayari upo ndani yako na hilo litakiwezesha kukipata kwa hakika.
Hatua za kuchukua;
Ni mara ngapi umekuwa unajiambia unajaribu kitu na uone kitaendaje? Ni matokeo gani umekuwa unayapata?
Kuanzia sasa achana na mambo ya kujaribu, fanya yale machache yanayotoka ndani yako kweli na weka kila ulichonacho ndani yako katika kufanya ulichochagua, utapata matokeo bora kuliko ambayo umekuwa unapata huko nyuma.
Tafakari;
Kujaribu kitu ni kuiambia asili kwamba hukitaki kweli kitu hicho. Na asili haina upendeleo, kama hunajitoa kweli kupata kitu, hutakipata.
Kocha.