2459; Siku Gani?
“Ipo siku yangu na mimi nitafanya makubwa.”
Sawa, tunakubaliana na wewe, lakini tuna swali kidogo; “ni siku gani hiyo?”
Kama huwezi kutujibu swali hilo, tafadhali usituhangaishe, kama umechagua kujidanganya mwenyewe ni sawa kwako, ila kuchagua kutudanganya na sisi siyo sawa.
Siku moja haijawahi kutokea, siku ambayo haijatajwa kwa hakika inaendelea kuwa na siku moja, ambayo huwa haifikiwi.
Kama kweli unataka kitu, lazima uweke mpango kamili wa kukipata na ufuate mpango huo.
Haijalishi kama utakipata kwa mpango huo, lakini kitendo cha kuwa na mpango unaoufanyia kazi, kinakusogeza karibu zaidi na kukipata.
Tofauti na wale wanaotamani tu, wanaojiambia wanakitaka kitu, ila hawajajitoa kwa namna yoyote ile ili kukipata.
Wewe kuwa tofauti, taka kitu ba jitoe kweli kukipata, usiishie tu kujifanganya mwenyewe na kuwadanganya wengi kuhusu siku moja ambayo ni ya kufikirika.
Hatua ya kuchukua;
Ni mara ngapi umekuwa unajiambia siku moja mambo yako yatakuwa mazuri?
Leo chukua hatua ya kuitaja siku hiyo na kuweka mpango unaofanyia kazi.
Kama umezama kwenye madeni yanayokutesa, usiseme tu siku moja yataisha, bali chagua siyo hiyo leo, labda mwaka mmoja au miwili ijayo na kisha andika tarehe na sema siku hiyo utakuwa huru kutoka kwenye madeni.
Kisha weka mpango wa jinsi utalipa madeni yako ili kufika siku hiyo uliyochagua yawe yameisha.
Kadhalika kwenye mengine unayotaka, iwe ni kufikia uhuru wa kifedha, kuanzisha na kukuza biashara n.k. Chagua siku kwa uhakika kabisa na weka mpango unaofanyia kazi.
Tafakari;
“Siku moja mambo yangu yatakuwa mazuri.” Ni kauli ambayo haijawahi kusemwa na mtu yeyote aliyewahi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Wote waliosema kauli hiyo waliishia kuwa kawaida.
Wale ambao wamefanikiwa, walijua kwa hakika nini wanataka, wanakitaka lini na wakaweka mpango walioufanyia kazi mpaka wakapata walichotaka.
Kocha.