2462; Ukiwa chini na ukiwa juu.

Unapokuwa chini, kuwa mtu wa shukrani.
Na unapokuwa juu, kuwa mnyenyekevu.
Hii ni kanuni muhimu ya maisha ambayo itakuwezesha kufanikiwa na kudumu kwenye mafanikio hayo.

Unapokuwa chini, pale mambo yanapokuendea vibaya ni rahisi kulalamika na kulaumu kwa nini hayo yawe hivyo kwako.
Lakini malalamiko na lawama hizo huwa hazina msaada wowote kwako. Badala yake mambo huzidi kuwa magumu.
Huo ni wakati mzuri wa kuwa mtu wa shukrani, kushukuru kwa mazuri uliyonayo kwenye maisha yako, kitu kitakachovuta mazuri zaidi yaje kwako.
Uzuri ni kwamba, hata mambo yawe mabaya kiasi gani, kuna mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako. Yatambue na ushukuru ili uweze kuvuta mengi zaidi kuja kwako.

Unapokuwa juu, pale mambo yanapokuendea vizuri ni rahisi kujisahau na kuona umeshajua na kuweza kila kitu. Ni rahisi kuwa na kiburi na majivuno kutoka na mambo yako kwenda vizuri.
Lakini asili huwa ina njia zake za kutushangaza. Ni pale unapodhani unajua kila kitu ndiyo asili inakuonyesha hakuna unachojua.
Hivyo unapokuwa juu, kuwa mnyenyekevu, jua kwamba unaweza kupoteza kila kitu na kurudi chini kabisa.
Hilo litakufanya uendelee kuweka juhudi na kuendelea kujifunza, vitu ambavyo vitakufanya uendelee kubaki juu.
Epuka sana kiburi na majivuno unayopata pale unapopiga hatua, vitu hivyo huharakisha anguko lako.

Hatua ya kuchukua;
Kika siku fanya zoezi la shukrani, kwa kuorodhesha mambo matatu mpaka matano unayoshukuru kuwa nayo kwenye maisha yako.
Kila wakati kuwa mnyenyekevu, ukijua hujui kila kitu wala hujapata kila kitu, jifunze na endelea kuweka juhudi zaidi kila wakati.
Kwa hatua hizo mbili, kuwa chini hakutakuwa milele na kuwa juu hutaanguka haraka.

Tafakari;
Mambo yanapokuwa mabaya, shukuru kwa mazuri mengine uliyonayo, shukrani huvuta mambo mazuri zaidi.
Mambo yanapokuwa mazuri, epuka kiburi na majivuno, hivyo huvuta anguko haraka.

Kocha.