2473; Uimara ndani ya udhaifu.

Tumeshajifunza sana jinsi ambavyo hakuna aliyekamilika.
Kwamba kila mmoja wetu ana madhaifu yake.

Wengi huwa wanalipokea hilo kwa mtazamo wa kuyaondoa madhaifu yao na ili yasiwe kikwazo.

Kinachotokea ni madhaifu yao yanazidi kuwa imara huku uimara wao ukiwa dhaifu.

Yaani unapoweka nguvu kuyaondoa madhaifu yako, unaishia kuyapa nguvu zaidi. Na kwa sababu huweki nguvu hizo kwenye uimara wako, unaunyima nguvu.

Kwenye kila udhaifu ulionao, kuna uimara ndani yake.
Hivyo badala ya kuhangaika kuondoa udhaifu ulionao, angalia ni uimara gani ambao uko ndani ya udhaifu huo na kisha utumie.

Labda huwezi kuongea mbele ya watu, lakini unaweza kuandika vizuri. Unaweza kutumia njia hiyo kuwasiliana vizuri kuliko kuongea.

Hata kwa watu unaoshirikiana nao, madhaifu yao yana uimara na manufaa ndani yake.
Labda ni mtu anayeongea sana, asiyeweza kukaa na kitu. Huyo ni mzuri pale unapohitaji taarifa fulani isambae kwa haraka.

Wanasema hata saa mbovu huwa inasema ukweli mara mbili kwa siku.
Hivyo madhaifu yoyote uliyonayo au waliyonayo wengine, usiyachukulie kama kikwazo pekee, bali angalia ndani yake, kuna uimara na manufaa pia.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini kwa madhaifu uliyonayo na ona ni kwa namna gani unaweza kuyatumia kwa manufaa. Hakuna udhaifu wowote usioweza kutumika kwa manufaa.
Pia kwa wale unaoshirikiana nao kwa namna mbalimbali, jua madhaifu yao na jinsi unavyoweza kuyatumia kwa manufaa.
Hakuna kisicho na matumizi, kiwe kizuri au kibaya.

Tafakari;
Kuweka nguvu kuyaondoa madhaifu yako ni kuyafanya yawe imara zaidi. Unachopaswa kufanya ni kuangalia jinsi ya kutumia madhaifu uliyonayo kwa manufaa, na hapo utaweza kufanya makubwa zaidi.

Kocha.