2474; Fanya vichache kwa ubora.
Moja ya sababu za wengi kushindwa kufanya wanayofanya kwa ubora ni kuhangaika na mambo mengi.
Watu wanakazana kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, kitu ambacho kinaathiri ufanisi wao.
Unapofanya mambo mengi kwa wakati mmoja, unatawanya sana nguvu na umakini wako na kuishia kupata matokeo ya kawaida tu.
Ukipunguza yale unayofanya na kuelekeza nguvu na umakini wako kwenye mambo machache, utayafanya kwa ubora wa hali ya juu.
Kupunguza mambo ya kufanya ni zoezi gumu kwenye zama hizi ambazo fursa mpya ni nyingi na zinakuja mpya kila siku.
Kwa kuwa mtu una kiu kubwa ya mafanikio, unaona hupaswi kupitwa na fursa hizo nzuri.
Lakini kinachotokea ni fursa hizo nyingi zinakupoteza badala ya kukusaidia.
Hapa kuna hatua tano za kuweza kupunguza yale unayofanya ili ubaki na machache ambayo utayafanya kwa ubora.
Hatua ya kwanza ni kuorodhesha mambo yote unayohangaika kuyafanya kwa sasa. Orodhesha yote na usiache hata moja.
Hatua ya pili ni kuchagua mambo machache katika hayo uliyoorodhesha, ambayo ukiyafanya vizuri utaleta matokeo makubwa na yatakayofidia mengine utakayoachana nayo.
Hatua ya tatu ni kuweka nguvu zako zote na umakini wako wote kwenye kifanya yale machache uliyochagua. Chagua kufanya kwa viwango vya daraja A kwenye hayo machache badala ya kufanya kwa viwango vya daraja B au C kwenye mengi.
Hatua ya nne ni kuachana kabisa na yale ambayo siyo muhimu kuhakikisha hayapati nguvu na umakini wako. Hata zinapokuja fursa nyingine mpya, hata kama ni nzuri kiasi gani, kama haziendani na yale machache uliyochagua, usihangaike nazo.
Hatua ya tano ni kujitoa kweli kweli kwenye yale machache uliyochagua, kuhakikisha unayafanya kwa ubora wa hali ya juu sana kuliko mwingine yeyote anavyoweza kuyafanya.
Kwa kufuata hatua hizo tano, utaweza kutumia nguvu zako na umakini wako kwenye kufanya mambo yenye tija na yanayozalisha matokeo bora.
Hatua ya kuchukua;
Fuata hizo hatua tano hapo juu kwenye yale unayofanya. Baki na machache ambayo utayafanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa. Na kisha weka kila ulichonacho kwenye yale machache uliyochagua.
Tafakari;
Mwanga wa jua ukitawanyika unatoa mwaka wa kawaida tu. Lakini mwanga huo huo ulikusanywa eneo moja unatoa moto mkali unaoweza kukata chuma. Hivyo pia ndivyo nguvu na umakini wako vilivyo. Ukitawanya sana vinakuwa kawaida, ukikusanya eneo moja vinakuwa na nguvu ya kufanya makubwa.
Kocha.