2475; Angalia Muda.
Tumekuwa tunaona jinsi watu wanalaghaiwa na kutapeliwa kwenye zama hizi.
Kwa kuitwa kwenye fursa mbalimbali ambazo zinawahamasisha kweli kweli na wanaziamini, lakini baadaye wanakuja kugundua wametapeliwa.
Nilishakushirikisha njia moja ya kupima kama fursa ni ya kweli au utapeli, ambayo ni kujiuliza kazi unayopaswa kuweka na thamani unayotoa.
Kama unaambiwa kuna fursa nzuri na inayolipa sana na ambayo haikuhitaji wewe kuweka kazi yoyote, pata wasiwasi, huenda wewe ndiyo fursa yenyewe.
Sasa kuna kigezo kingine cha kuangalia ili kujua kama fursa ni ya kweli au utapeli.
Kigezo hicho ni muda.
Kama unaambiwa fursa inaanza kukulipa mara moja, yaani ndani ya muda mfupi kuwa na wasiwasi.
Mambo yote mazuri na yenye manufaa makubwa huwa yanahitaji muda kujengwa.
Hakuna njia ya mkato kwenda kwenye ubora na mafanikio makubwa.
Hivyo unapoona watu wanakuita kwenye fursa ambayo manufaa yake ni ya haraka, jua haina thamani kubwa kama wanavyokuambia au wanataka tu kukutapeli.
Hitaji la muda ni kanuni ya asili kabisa.
Mchicha unaota ndani ya muda mfupi na kufa ndani ya muda mfupi pia.
Mbuyu unachukua miaka kuota lakini unadumu miaka mingi.
Kadhalika kwenye maisha yetu, mambo yote mazuri yanahitaji muda, tena ambao huwezi kuukatisha.
Mimba inayohitaji miezi tisa ya kukaa tumboni, huwezi kufupisha hilo bila ya madhara.
Malezi yanahitaji muda, siyo kitu cha mkato.
Kujenga taaluma, ujuzi na hata biashara kunahitaji muda, huwezi kufanya hilo haraka.
Lakini cha kushangaza, bado watu wanahangaika na njia za mkato, njia ambazo hazifanyi kazi, lakini bado hawaziachi.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila kitu unachoshawishika kufanya, angalia ni muda kiasi gani unaohitajika kwenye kukijenga, kisha wekeza muda huo kwenye kukijenga.
Unapoona fursa unaambiwa ni ya haraka, ya njia za mkato na isiyohitaji muda, pata wasiwasi, hakuna fursa hapo.
Tafakari;
Mambo yote makubwa na muhimu yanahitaji muda, ndiyo maana wengi huwa hawawezi kuyafanya na hilo kuwa kikwazo kwa mafanikio yao.
Wewe kuwa tayari kuweka muda wa kutosha kwenye kitu ili kuweza kuzalisha matokeo makubwa.
Kocha.
Asante Sana kocha, Nashukuru kwa kigezo hiki cha muda. Ni kweli kabisa kila kitu chenye manufaa kinahitaji muda. Ninajisukuma kuweka muda, Kazi na umakini wangu kwenye kile nilichochagua kufanya.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike