2476; Nipe Nikupe.

Nipe nikupe ni mtazamo mbovu sana ambao umekuwa kikwazo kwa wengi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao.

Wengi hawapo tayari kutoa kitu, mpaka wawe na uhakika wa kupata kitu.
Au mbaya zaidi watu wanasubiri mpaka wapate ndiyo nao watoe.

Mtu anasubiri mwajiri wake amwongezee mshahara ndiyo afanye kazi kwa kujituma.
Mwingine anasubiri wateja wawe tayari kulipa zaidi ndiyo awape huduma bora.

Yote hiyo ni kinyume kabisa na kanuni za asili na ndiyo maana watu hawafanikiwi kwa kufanya hivyo.

Huwezi kwenda kwenye shamba na kuliambia nipe kwanza mazao kisha nitakupa mbegu.
Huwezi kuweka kuni jikoni na kuziambia ziwake kwanza ndiyo utazipa moto.

Asili haifanyi kazi hivyo, hupati kwanza ndiyo ukatoa, bali unatoa kwanza kisha ndiyo unapata.
Na tena hutoi kwa sababu unategemea kupata, bali unatoa kwa sababu umechagua kutoa.
Unapotoa kwa moyo mmoja bila kujali unapata nini, unajikuta ukipata kwa wingi zaidi.

Asili huwa haipendi kuwa na deni na pia huwa haipendi utupu. Hivyo hujaza popote palipopungua na kujaza kwa viwango vya juu kabisa.

Hivyo badala ya kusubiri mwajiri akulipe zaidi ndiyo ujitume kwenye kazi, anza kujituma na utaona jinsi mwajiri atakavyokuwa tayari kukulipa. Na kama yeye hatajali kukulipa, kuna wengine wataona juhudi zako na kuwa tayari kukulipa zaidi.

Badala ya kusubiri wateja wawe tayari kulipa zaidi ndiyo uwape huduma bora, anza kutoa huduma bora na utaona jinsi wateja watakuwa tayari kukulipa zaidi.

Kwa kusikia hivi roho ya uhaba ndani yako itakuwa inakuambia watu hawajali, unaweza kutoa sana na bado wasikupe.
Na roho hiyo ndiyo imekuwa kikwazo kwako mpaka sasa, lazima uiondoe kama unataka mafanikio.

Hebu fikiri, kama unafanya kazi masaa 8 kila siku, kuna tofauti gani kwako ukitumia masaa hayo kufanya kazi bora kabisa au ya hovyo? Je ni bora uendelee kufanya kazi ya hovyo na kubaki hapo au kufanya kazi bora yenye fursa ya wewe kupiga hatua zaidi?

Kama unawahudumia wateja wako kwa bidhaa ile ile na muda ule ule, je ni bora uwahudumie hovyo na uwe kwenye hatari ya kuwapoteza au uwahudumie vizuri na uwe kwenye fursa ya kubaki nao na kuwavutia wengine zaidi?

Juhudi ni zile zile, muda ni ule ule, ni wewe tu unayechagua namna unavyotumia.
Chagua kutoa thamani kubwa zaidi kwenye kila unachofanya, thamani kubwa kuliko wengine wanavyotegemea na usiangalie sana unachopata, wewe angalia zaidi unachotoa.

Kanuni ya asili ambayo huwa haishindwi, italeta vitu vizuri sana kwako kwa sababu umekuwa tayari kutoa.
Lakini wewe toa kwa sababu ndiyo wajibu wako na siyo kwa sababu unategemea kupata kitu fulani.
Ukishaweka mategemeo yako tu, jua umeshaharibu.

Hatua ya kuchukua;
Kwa shughuli yoyote unayofanya, iwe ni kazi au biashara, kila siku chagua kwenda hatua ya ziada. Chagua kutoa thamani kubwa kuliko unavyotegemewa kutoa.
Fanya hivyo kwa sababu ndiyo msingi uliochagua kuuishi. Haitachukua muda mrefu utaanza kuvuna matunda yake.
Lakini wewe fanya kwa sababu umechagua kufanya na siyo kwa sababu kuna kitu unategemea kupata.

Tafakari;
Mtazamo wa uhaba umekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa, kwa sababu wamekuwa hawapo tayari kutoa mpaka wapate.
Dunia ina utele, walio na mtazamo wa utele, ambao wapo tayari kutoa bila kuangalia wanachopata ndiyo wanaokuwa kwenye fursa ya kupata zaidi.

Kocha.