2477; Hakuna nguvu za ziada.
Moja ya kanuni muhimu niliyojifunza kwenye fizikia na ambayo inaendana sana na maisha ya mafanikio ni kuhusu nguvu.
Kanuni ya nguvu kwenye fizikia inasema nguvu haiwezi kuzalishwa wala kuharibiwa, bali inaweza kubadilishwa kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine.
Kwa mfano gari iliyo kwenye mwendo ina nguvu ya mwendo. Ikigonga ukuta na kusimama, nguvu ile ya mwendo haijaharibiwa au kupotea, badala yake inakuwa imebadilishwa kuwa nguvu nyingine, kama sauti, uharibifu na joto.
Ile sauti inayosikika gari linapogonga kitu ni sehemu ya nguvu ya mwendo imebadilishwa.
Uharibifu unaotokea kwenye gari au kile kilichogongwa ni sehemu ya nguvu iliyobadilishwa.
Ndiyo maana gari inayoenda kwa kasi kubwa itatoa sauti kubwa na uharibifu wake pia utakuwa mkubwa kwa sababu nguvu inayobadilishwa ni kubwa pia.
Sasa tuje kwenye maisha ya mafanikio.
Nguvu binafsi ulizonazo kwenye siku yako ni kiwango kile kile, hakuna cha ziada.
Unapotumia nguvu hizo kwenye kitu kimoja, huwezi kuzitumia tena kwenye kitu kingine.
Ndiyo maana huwa unaimaliza kila siku ukiwa umechoka, iwe umefanya kazi ya maana au kazi ya hovyo.
Kama unaweka nguvu zako kwenye kupinga au kubomoa kitu, jua huwezi kutumia nguvu hizo kukubali au kujenga kingine. Je ni upande upi wenye manufaa kwako?
Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu zao bila ya kujua hilo na hivyo kujikuta wakiwa kikwazo kwa mafanikio yao wenyewe.
Mfano unapotumia nguvu kuonyesha wengine wamekosea, hizo ni nguvu ambazo huwezi kuzitumia kuonyesha kile kilicho sahihi.
Unapotumia nguvu kuwashambulia washindani au wakosoaji wako, hizo ni nguvu ambazo huwezi kutumia kuonyesha utofauti na upekee wako.
Unaweza kushangaa mbona watu wawili wanaweza kuwa wanafanya kazi au biashara ya aina moja, mmoja akafanikiwa na mwingine akashindwa. Jibu lipo kwenye vipaumbele na matumizi ya nguvu.
Japo kwa nje wataonekana kufanya vitu vinavyofanana, uwekezaji wao wa nguvu ni tofauti na hivyo matokeo pia yanakuwa tofauti.
Hatua ya kuchukua;
Jitathmini jinsi umekuwa unatumia nguvu zako kila siku. Je uwekezaji mkubwa unafanya wapi, kwenye kujenga au kubomoa. Peleka nguvu zako kwenye kujenga kile unachotaka kuliko kubomoa usichotaka au wengine. Nguvu zina uhaba na ukomo, zitumie kwa namna ambayo zitakuwa na marejesho mazuri kwako.
Tafakari;
Kila unapochagua kufanya jambo moja, jua umechagua kutokufanya jambo jingine. Hivyo kwa kila jambo unalochagua kufanya, jiulize je hicho ndiyo kipaumbele kikubwa kwako? Hayo ndiyo matumizi bora kabisa ya nguvu zako kwa wakati huo? Usifanye tu kwa mazoea, wekeza nguvu zako kimkakati.
Kocha.