2484; Viongozi na wafuasi.

Viongozi hawatengenezi wafuasi, bali wanawakusanya.
Wafuasi wanakuwepo tayari, wakiwa na mahali wanataka kwenda.
Pale wanapomuona mtu ambaye anaweza kuwaongoza kufika kule wanakotaka kufika, wanakuwa tayari kumfuata.

Wafuasi hawamfuati kiongozi kwa sababu tu anataka kuwaongoza.
Bali wafuasi wanamfuata kiongozi kwa sababu ya maono aliyo nayo na yale anayosimamia.

Kila mmoja wetu ana nafasi ya uongozi kwenye maisha, kazi na biashara tunazofanya.
Kama viongozi tunapenda kuwa na wafuasi.
Tunachopaswa kujua ni watu hawatatufuata kwa sababu tunataka watufuate.
Badala yake watu watatufuata kwa sababu kuna mahali wao wanataka kufika.

Kwa maneno mengine watu wanatufuata siyo kwa sababu zetu wenyewe, bali kwa sababu zao wenyewe.
Hivyo ili kuwa kiongozi bora, lazima ujue wale unaotaka kuwaongoza wanataka nini na kisha kuwapatia.

Wakati mwingine watu hao hawajui nini hasa wanachotaka, lakini hawataki kubaki pale walipo sasa. Hivyo ni wajibu wako kama kiongozi kuwawezesha kufika zaidi ya pale walipo sasa.

Kama kiongozi unahitaji vitu vikubwa viwili.

Kwanza unahitaji kuwa na maono makubwa ya wapi unaelekea. Maono hayo ndiyo yanawafanya wafuasi waje kwako, kwa sababu nao kuna mahali wanataka kufika.

Pili unahitaji kuwa na falsafa unayoiishi na kuisimamia. Falsafa ndiyo inakupa msimamo wa nini unafanya na nini hufanyi. Bila falsafa utapata wafuasi wasio sahihi na pia utawapoteza wafuasi wengi kwa sababu hawajui unasimamia upande upi.

Hatua ya kuchukua;
Ni maeneo gani unayotaka kuwa kiongozi bora? Tengeneza maono makubwa na falsafa unayoiishi, hivyo vitawaleta wafuasi sahihi kwako.
Ni viongozi gani unawahitaji ili kufika unakotaka? Angalia maono na falsafa zao ili kujua walio sahihi kwako.

Tafakari;
Hakuna uhaba wa wafuasi, bali kuna uhaba wa viongozi. Kuwa kiongozi sahihi na wafuasi sahihi watakuja kwako.

Kocha.