2484; Viongozi na wafuasi.
Viongozi hawatengenezi wafuasi, bali wanawakusanya.
Wafuasi wanakuwepo tayari, wakiwa na mahali wanataka kwenda.
Pale wanapomuona mtu ambaye anaweza kuwaongoza kufika kule wanakotaka kufika, wanakuwa tayari kumfuata.
Wafuasi hawamfuati kiongozi kwa sababu tu anataka kuwaongoza.
Bali wafuasi wanamfuata kiongozi kwa sababu ya maono aliyo nayo na yale anayosimamia.
Kila mmoja wetu ana nafasi ya uongozi kwenye maisha, kazi na biashara tunazofanya.
Kama viongozi tunapenda kuwa na wafuasi.
Tunachopaswa kujua ni watu hawatatufuata kwa sababu tunataka watufuate.
Badala yake watu watatufuata kwa sababu kuna mahali wao wanataka kufika.
Kwa maneno mengine watu wanatufuata siyo kwa sababu zetu wenyewe, bali kwa sababu zao wenyewe.
Hivyo ili kuwa kiongozi bora, lazima ujue wale unaotaka kuwaongoza wanataka nini na kisha kuwapatia.
Wakati mwingine watu hao hawajui nini hasa wanachotaka, lakini hawataki kubaki pale walipo sasa. Hivyo ni wajibu wako kama kiongozi kuwawezesha kufika zaidi ya pale walipo sasa.
Kama kiongozi unahitaji vitu vikubwa viwili.
Kwanza unahitaji kuwa na maono makubwa ya wapi unaelekea. Maono hayo ndiyo yanawafanya wafuasi waje kwako, kwa sababu nao kuna mahali wanataka kufika.
Pili unahitaji kuwa na falsafa unayoiishi na kuisimamia. Falsafa ndiyo inakupa msimamo wa nini unafanya na nini hufanyi. Bila falsafa utapata wafuasi wasio sahihi na pia utawapoteza wafuasi wengi kwa sababu hawajui unasimamia upande upi.
Hatua ya kuchukua;
Ni maeneo gani unayotaka kuwa kiongozi bora? Tengeneza maono makubwa na falsafa unayoiishi, hivyo vitawaleta wafuasi sahihi kwako.
Ni viongozi gani unawahitaji ili kufika unakotaka? Angalia maono na falsafa zao ili kujua walio sahihi kwako.
Tafakari;
Hakuna uhaba wa wafuasi, bali kuna uhaba wa viongozi. Kuwa kiongozi sahihi na wafuasi sahihi watakuja kwako.
Kocha.
Hongera kocha Dr Amani kwa kuwa kiongozi wa kisima cha maarifa,na kuweka wazi maono ya kisima cha maarifa kwetu sote.Kwa umri wako tunashukuru Mungu kwa kukupa maono haya ambayo ni chachu ya kila mmoja wetu kwenye kisima cha maarifa anatamani kuyafikia.
Maadam sote wanachama kisima cha maarifa tuna maono yanayorndana na kiongozi wetu ni jukumu letu kuifuata falsafa ya kisima cha maarifa iliyopo.
LikeLike
Asante Kocha,
Jumapili ya kuhitimisha semina ya KCM 2021 pale Dodoma tulikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana. Baada ya mazungumzo ulipenda nizungumze jambo lolote, nikachagua matembezi/mchakamchaka tuliokuwa tumefanya asubuhi hiyo, jumapili. Kwa maoni yangu Wazo hilo lilipokolewa vizuri sana na wanasemina. Nilikushirikisha kwamba wazo hilo katika mazingira ambayo si tofauti sana na pale Dodoma halikupokelewa vyema, ingawa lengo ni lile lile. Nilikuuliza nini SIRI? Ulinijibu kwa kuongelea uongozi (leadership).
Makala hii umeingia ndani, nimeelewa kiongozi ni kuwa na maono na kuweza kuyatafsiri na kuyasimamia. Kiongozi bora hatafuti wafuasi. Wafuasi ndiyo humtafuta kiongozi kwa sababu wafuasi wa kweli wanahitaji kiongozi bora.
Ninashukuru kocha kwa hili.
LikeLike
Asante sana Mzee Mbise,
Kweli kabisa ni katika mazungumzo haya ndipo nikaupata ukurasa huu.
Kila mmoja wetu akitambua uongozi wake na kusimamia maono na falsafa, wafuasi watakuja kwa sababu ya vitu hivyo.
LikeLike
Asante sana Hendry,
Karibu tuendelee kuwa pamoja katika safari hii.
LikeLike
Ni ukweli kwamba wafuasi wapo wengi lakini kinachokosekana ni viongozi bora. Jukumu langu kubwa ni kukazana kuwa kiongozi bora ili kuwafutia wafuasi bora kabisa tutakaoweza kwenda nao kwenye safari hii ya kufikia Mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Asante Sana kocha kwa makala hii.
LikeLike