2488; Afya ya hisia.
Tumezoea afya ya akili, mwili na roho.
Lakini inapokuja kwa hisia, huwa hatupendi kuziongelea.
Kwa kuona hisia ni udhaifu.
Lakini sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia kisha kuyahalalisha kwa fikra.
Hivyo kama hatutakuwa na afya nzuri ya kihisia, tutaishia kufanya maamuzi mabovu na ambayo yatakuwa kikwazo kwa mafanikio yetu.
Kuahirisha mambo ni matokeo ya hisia tunazokuwa nazo.
Na hata mambo ya hovyo tunayofanya, tunasukumwa na hisia.
Kama tunataka kufanya maamuzi bora, kuwa na msukumo wa kufanya makubwa na kuwa na ubunifu mkubwa, tunahitaji kuwa na afya bora ya hisia.
Kujenga afya yako ya hisia unapaswa kutokuzikimbia au kuzikandamiza hisia zako.
Hicho ndiyo wengi hufanya, pale hisia fulani zinapowajia, wanazikimbia au kuzikandamiza kwa sababu hawataki kuonekana dhaifu.
Lakini hisia zina nguvu kubwa, hata kama zitakandamizwa, hazitazimika kabisa, badala yake zinaendelea kupata nguvu na siku moja zinakuja kuibuka kwa ukali na kuleta madhara.
Umewahi kufanyiwa kitu kidogo lakini ukawa na hasira kali sana, hasira zisizoendana kabisa na kilichofanyika? Jua kitu hicho kimeenda kutonesha hisia fulani ambazo ulikuwa umezikandamiza.
Kuondokana na hali za aina hiyo, jenga afya bora ya hisia zako.
Unaijenga afya ya hisia kwa kutokuzikimbia au kuzikandamiza hisia unazokuwa nazo.
Badala yake kaa nazo kwa muda, jua chanzo chake, jua kwa nini hisia hizo zimeibuka na uzitatue ili zisiendelee kukua zaidi.
Hii haimaanishi usukumwe na hisia hizo kufanya mambo ambayo baadaye utayajutia.
Bali inamaanisha kuzitambua hisia zako na kuelewa kwa nini zinakuja kwako na namna gani ya kuzuia zisije tena kama ni hasi au namna ya kuzitumia kama ni chanya.
Unapozikimbia au kuzikandamiza hisia zako, unahitaji nguvu kubwa ya kuendelea kuzikandamiza, nguvu ambayo huwezi kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Unapozikabili hisia zako na kuzitatua, nguvu yako inakuwa huru kutumika kufanya makubwa zaidi na hivyo kuweza kufanikiwa.
Hisia zina nguvu kubwa ambayo ukiweza kuitumia vizuri utaweza kufanya makubwa zaidi. Lakini hayo yote yanaanza na kuwa na afya bora ya hisia. Kwa kuzitambua hisia zako, kuzitatua na kutumia nguvu yake kufanya makubwa.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapopatwa na hisia ambazo haziendani na tukio husika, jua ni hisia ambazo umekuwa unazikandamiza kwa muda mrefu. Usiendelee tena kuzikandamiza, badala yake chimba ndani na ujue chanzo chake, kisha tatua ili uwe huru.
Mfano umekutana na mtu mliyesoma naye na ukaona amepiga hatua kuliko wewe, unajikuta ukipatwa na wivu na chuki.
Usiishie tu kukandamiza hisia hizo na kujilazimisha kuyafutaria mafanikio yake. Bali jiulize kwa nini umepatwa na hisia hizo. Labda hujiamini au hujikubali kwa vile ulivyo. Labda unajilinganisha sana na wengine na kukazana kuwa kama wengine badala ya kuwa wewe.
Kwa kukaa na hisia za aina hiyo, utakijua chanzo na hivyo kutatua ili wakati mwingine usisumbuke tena.
Tafakari;
Sisi binadamu kama viumbe wa hisia tunaweza kufanya makubwa sana kama tutakuwa na afya nzuri kihisia. Unapokuwa na hisia hasi jua chanzo chake na ukitatue. Unapokuwa na hisia chanya pia zitumie kufanya makubwa.
Hofu ni hisia hasi, unapojua chanzo chake utaweza kuitatua na kufanya makubwa.
Upendo ni hisia chanya, unapoutumia vizuri unaweza kufanya makubwa.
Kocha.
Asante Sana kocha, nahitaji mno afya ya hisia ili kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yangu.
LikeLike
Sawa, fanyia kazi hilo.
LikeLike