2490; Kama inabidi utumie nguvu sana, kuna kitu hakipo sawa.

Kama inabidi utumie nguvu nyingi kuwaonyesha watu umefanikiwa, jua hujafanikiwa.

Kama inabidi utumie nguvu kubwa kuwaonyesha watu kwamba wewe ni mwaminifu, basi siyo mwaminifu.

Kama inabidi uwalazimishe watu kuuona ukweli, huo utakuwa siyo ukweli.

Kama kila wakati unajiuliza iwapo una furaha au la, huna furaha.

Na kama unatumia nguvu nyingi kupenda kile unachofanya, basi hukipendi kweli.

Ndani yetu tunajua kilicho kweli na sahihi, lakini tumekuwa tunapuuza na kuhangaika na nguvu.
Kitu ambacho kinatuchosha sana na kutuzuia tusifanikiwe.

Huhitaji kutumia nguvu kubwa sana kwenye yale yaliyo sahihi, yanapaswa kuwa sehemu ya maisha yako, kama ilivyo kupumua au kumeng’enya chakula.

Ukishajiona unatumia nguvu kupumua au kumeng’enya chakula, jua mwilo haupo sawa, utakuwa unaumwa.
Kadhalika ukijiona unatumia nguvu nyingi kwenye eneo lolote la maisha yako, kuna kitu hakipo sawa kwenye eneo hilo.

Hatua ya kuchukua;
Angalia kila eneo la maisha yako na ona ni maeneo gani umekuwa unatumia nguvu kubwa kuliko kawaida.
Chochote kile unachokiwekea nguvu sana, maana yake kuna kitu hakipo sawa.
Jua kile ambacho hakipo sawa na ukibadili ili uweze kutumia nguvu zako kwa mambo sahihi na siyo kuhangaika na yasiyo sahihi.

Tafakari;
Maji huwa yanafuata mkondo wake bila kutumia nguvu kubwa. Ni pale unapotaka kuyapeleka maji tofauti na mkondo wake ndiyo unahitaji kutumia nguvu kubwa. Kama unahitaji nguvu kubwa kwenye kitu, jua kipo nje ya mkondo wake.

Kocha.