2491; Hawabadiliki, wanachoka kuigiza.
Watu huwa hawabadiliki, bali wanachoka kuigiza.
Angalau siyo kwa haraka kiasi hicho, yaani hata kama watu watabadilika, haiwi haraka na rahisi.
Hivyo unapojiambia mtu amebadilika, kuwa makini, mara nyingi anakuwa amechoka kuigiza na kuamua kuishi uhalisia wake.
Kwamba mtu alikuwa mwaminifu na ghafla amekuwa siyo mwaminifu tena. Kwa sehemu kubwa huyu mtu kutokuwa mwaminifu ndiyo ilikuwa tabia yake, ila aliamua kuigiza uaminifu. Sasa kwa kuwa maigizo yanahitaji nguvu, anafika mahali na kuchoka kuigiza, hivyo anarudi kwenye uhalisia wake.
Wakati mwingine madaraka au mafanikio yanaweza kumfanya mtu aache kuigiza. Wengi wakiwa chini na hawana nafasi wanaweza kuonekana ni wema na wanaojali. Lakini wanapofika juu au kuwa na nafasi ndiyo uhalisia wao unaonekana.
Ni rahisi kuigiza ukiwa chini na huna nafasi kuliko ukiwa juu na ukiwa na nafasi.
Kitu kingine ambacho nimewahi kuandika kwenye hizi kurasa na ambacho nataka kukukumbusha tena leo ni hiki; watu wakikuonyesha uhalisia wao, usiwakatalie.
Kuna wakati unataka sana kuwa na mtu halafu akaonyesha tabia ambayo ni kikwazo kwako. Kwa sababu unataka sana kuwa naye, unajifanya kama hujaona tabia hiyo au kama ni bahati mbaya tu kwa upande wake.
Zinduka kwenye hilo, mtu amekuonyesha mwenyewe, ya nini umkatalie?
Ubishi wako ndiyo unaokuja kuleta matatizo makubwa baadaye.
Hatua za kuchukua;
Umekuwa unashirikiana na watu mbalimbali ambao mwanzoni walionekana wako vizuri, lakini baadaye wakabadilika. Yale siyo mabadiliko bali ni mwisho wa maigizo.
Jifunze kuwa vizuri kwenye kuyajua maigizo ili usiwaamini watu wasiokuwa sahihi.
Tafakari;
Unahitaji muda ili kuweza kuwajua watu kwa undani. Mambo yakiwa mazuri wanaweza kuigiza, lakini mambo yanapokuwa tofauti au magumu, maigizo yanawashinda. Watu wanapokuonyesha uhalisia wao usiwakatalie, ndivyo walivyo.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike
Karibu
LikeLike