2494; Kuna neno hajasikia.
Nikiwa kwenye sherehe fulani, mshereheshaji alikuwa anatumia njia mbalimbali kuwashawishi watu kutoka kwenye viti na kwenda kucheza muziki.
Kwanza alianza kwa kutumia kigezo cha kupendeza, akisema wote mmependeza sana, na kwa kupendeza huko mje kucheza.
Akaona siyo wengi wanaotoka kucheza, akasema wale ambao hawatoki hawajapendeza. Bado hakupata mwitikio mkubwa.
Akatumia mbinu nyingine ya wenza, kwamba kila mmoja na mwenza wake watoke kucheza. Bado siyo wengi waliotoka.
Aliendelea kutumia mbinu nyingine kama vijana na wazee, na hii pia iliongeza watu kwa kiasi fulani.
Kilichonishangaza ni pale alipotumia mbinu ya timu za mpira, simba na yanga. Watu walitoka zaidi kwenda kucheza kwa kushindanishwa kitimu. Kwamba mashabiki wa timu ipi watawashinda wengine.
Kitu kikubwa cha kujifunza hapa ni kama kuna kitu unawashawishi watu wafanye na hawachukui hatua, siyo kwa sababu hawaelewi, ila kuna neno hawajasikia kutoka kwako.
Kuna neno moja tu wakilisikia, watachukua hatua mara moja.
Hivyo wajibu wako ni kujua kile ambacho unaowashawishi wanataka kukisikia na kuhakikisha unawaeleza ili wawe tayari kuchukua hatua.
Kumbuka kama una kitu kizuri na chenye manufaa kwa wengine, ni wajibu wako kuhakikisha wanajua uwepo wa kitu hicho na wanasukumwa kuchukua hatua.
Usijiambie kwamba umeshaeleza sana ila tu watu hawaelewi, usirudie kueleza yale yale, badili kulingana na aina tofauti za watu unaowalenga.
Hili ni muhimu sana kwenye masoko na matangazo mbalimbali tunayofanya kwenye kile tunachofanya.
Tusichoke kuwaelewesha watu, tusirudie kile kile, tujue watu kuna kitu wakisikia watachukua hatua, tuwaambie hicho.
Hatua za kuchukua;
Kwenye chochote unachowashawishi watu, jua aina tofauti za watu unaowalenga na kile wanachotaka kusikia ili wawe na uhakika wa kuchukua hatua.
Kuna ambao wanataka kupata uhakika wa kile unachowashawishi
Kuna ambao wanataka kuona wengine ambao wameshawishika.
Kuna ambao wanasubiri mpaka dakika za mwisho.
Na kuna ambao wanataka hali ya mashindano.
Usitoe ujumbe wa aina moja pekee, toa jumbe za aina tofauti ili kuwa na ushawishi kwa wengi zaidi.
Tafakari;
Watu hushawishika kwa njia tofauti tofauti, kulingana na kile wanachotaka wao wenyewe. Kama bado hujaweza kuwashawishi watu, jua hujaweza kuwaeleza kile wanachotaka kusikia.
Kocha.
Hii mbinu safii sana.
Nashukuru kocha kwa makala hii.
LikeLike
Karibu Sebastian.
LikeLike
Mbinu bora kocha,kuna Neno bado hawajasikia wateja wangu ili wachukue hatua ya kununua, asante kocha kwa makala hii.
LikeLike
Karibu.
LikeLike