#SheriaYaLeo (1/366); Gundua Wito Wako.

Ndani yako una nguvu kubwa inayokuongoza na kukusukuma kuelekea kwenye wajibu mkuu wa maisha yako.
Umekuja hapa duniani ukiwa na wajibu maalumu, wa jukumu kubwa unalopaswa kukamilisha katika miaka utakayoishi.

Ulipokuwa mtoto, nguvu hiyo ilikuwa wazi kabisa kwako. Ilikuelekeza kufanya vitu vinavyoendana na asili yako, vilivyoibua udadisi ndani yako.
Lakini kadiri ulivyokua, nguvu hiyo ilififia kutokana na kusikiliza watu mbalimbali kwa yale waliyokuwa wanakuambia pamoja na changamoto mbalimbali za maisha.

Kwa kuwa watu hao hawajui uwezo wako wa ndani na upi wajibu wako mkuu kwenye maisha, walikuondoa kwenye njia yako kuu.
Kilichotokea ni umejikuta kwenye maisha yasiyo na mwelekeo na hicho ndiyo chanzo kikuu cha kukosa furaha kwenye maisha yako.
Kwa kukosa muunganiko na ile nguvu kuu ya maisha yako, umejipoteza mwenyewe na kupotea njia ya maisha yako.

Hatua ya kwanza kuelekea ubobezi na mafanikio makubwa kwenye maisha yako ni kuanzia ndani yako, kujitambua wewe mwenyewe na kuunganika tena na nguvu kubwa iliyo ndani yako.
Kwa kuitambua nguvu hiyo kwa uhakika utaweza kujua kipi sahihi kwako kufanya na kuweza kupata mafanikio makubwa.

Kwa kujiunganisha tena na nguvu kuu iliyo ndani yako, mambo mengine yote yatakaa sawa kwenye maisha yako.
Hujachelewa, katika wakati wowote wa maisha yako unaweza kuanza mchakato huu wa kugundua wito na wajibu mkuu wa maisha yako, ukaanza kuuishi na kuwa na maisha bora.

Sheria ya leo; Mafanikio ni mchakato na kugundua wito wako ndiyo hatua muhimu ta kuanzia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma