Rafiki yangu mpendwa,
Heri ya mwaka mpya wa mafanikio 2021/2022.

Ninayo furaha ya kipekee kabisa kukukaribisha kwenye mwaka wetu huu mpya wa mafanikio, mwaka ambao tumejitoa kweli kweli kwenda kufanya makubwa.

Ni mwaka ambao lengo la kila mmoja wetu kubwa ni kukuza utajiri wake mara mbili ya ule alio nao sasa.
Na hivyo kila mmoja ana mpango na mkakati wa kufanyia kazi kila siku ili kuweza kufikia hilo.

Huu ni mwaka wa kazi, mwaka wa kujituma zaidi na mwaka wa kuweka umakini kwenye mambo machache na muhimu badala ya kutawanya umakini kwenye mambo mengi yasiyo muhimu.

Tunauanza mwaka wetu wa mafanikio leo tarehe 01/11/2021 na tunakwenda nao mpaka wiki ya mwisho ya oktoba 2022.

Kama ambavyo nimekuwa nashirikisha, mwaka huu nimejitoa kweli kufanya kazi kwa karibu na kila mwanamafanikio mpaka kuhakikisha kweli kwamba anapiga hatua na kuyabadili maisha yake.

Karibu sana utumie fursa hii vizuri, amua kujitoa kweli kwenye huu mwaka ili uweze kuzalisha matokeo ya tofauti kabisa kwenye maisha yako.
Kitu ambacho kinawezekana kabisa kama utachagua kufanya tofauti na ambavyo umekuwa unafanya.

Ahadi ambayo nimeitoa ni kwamba nitamsumbua sana kila mtu katika kuhakikisha anaifuata misingi sahihi ya mafanikio.
Kwa sababu najua ukiifuata misingi, matokeo mazuri lazima yaje, siyo kwa kubahatisha, bali kwa uhakika.

Rafiki, mwaka ndiyo huu umeshaanza na moto tuliouwasha haupaswi kupoa wala kuzima. Wajibu wetu ni kuendelea kuuchochea ili ulete matokeo makubwa zaidi.

Nikutakie kila la kheri kwenye mwaka wetu huu mpya wa mafanikio, uende ukawe mwaka wa kupindua meza kwako, wa kuyabadili kabisa maisha yako na kuyaweka kwenye mwelekeo sahihi.

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.