#SheriaYaLeo (6/366); Mabadiliko Ni Sheria.
Mabadiliko ni sheria ya maisha.
Hakuna kitu chochote kinachobaki kilivyo, kila kitu kinabadilika.
Katika kukabiliana na mabadiliko kwenye kazi na biashara zako, endana na mabadiliko badala ya kuyapinga.
Tambua kwamba hujafungiwa kwenye kufanya kitu cha aina fulani pekee.
Uaminifu wako siyo kwenye kazi, biashara au taasisi unayofanya nayo kazi.
Bali uaminifu wako unapaswa kuwa kwenye kusudi na wajibu mkuu wa maisha yako.
Unachopaswa ni kuliishi kusudi lako kwa ukamilifu wake, kutekeleza wajibu wako mkuu.
Hivyo kuwa tayari kutumia kila njia na kila fursa inayojitokeza mbele yako kukamilisha hilo.
Manadiliko yanapotokea siyo mwisho wa kusudi na wajibu wako, bali unapaswa kutumia njia nyingine kuendelea na kusudi na wito wako.
Mlango mmoja unapojifunga, jua kuna milango mingine ambayo iko wazi kwa ajili yako.
Mabadiliko hayakwepeki, hasa kwa zama hizi za kimapinduzi tunazoishi sasa.
Ni wajibu wako kuyaona mabadiliko mapema kabla hayajafikiwa na kuanza kubadilika mapema ili uendelee kufanyia kazi kusudi na wito wako.
Using’ang’ane na mambo ya nyuma hata kama yalifanya kazi vizuri.
Mabadiliko hayawezi kuzuiliwa au kukwepwa, ni lazima uyakabili kama unataka kuendelea na kusudi na wajibu wa maisha yako.
Sheria ya leo; Badili mwelekeo wako kulingana na mabadiliko yanayoendelea kutokea. Epuka kuwa na malengo na mipango mgando. Muhimu kwako ni kuishi kusudi lako na kutekeleza wajibu wako mkuu, badilika kadiri inavyohitajika ili kutimiza hilo. Mabadiliko ni sheria.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma