2504; Jenga Mahusiano Zaidi.

Huwa kuna kauli kwamba haijalishi unajua nini, bali unamjua nani.
Sehemu kubwa ya mafanikio yako inatokana na wale unaowajua kuliko yale unayoyajua.

Hii ni kusema kwamba mahusiano yako na watu sahihi ni muhimu sana kwenye mafanikio yako.
Kwa sababu kama unavyojua, kila unachokihitaji tayari kipo kwa watu wengine.

Kazi na biashara unayoifanya ni watu wengine wana mahitaji nayo.
Kadiri unavyoweza kuwafikia wengi zaidi, ndivyo unavyoweza kufanya kwa ukubwa zaidi na kupata manufaa zaidi.

Watu unaohitaji kuwafikia wanaweza kuwa wanajuana na watu unaowajua. Watu hao wanaweza kurahisisha zoezi la wewe kuwafikia unaowataka.

Una wajibu mkubwa wa kujenga mahusiano sahihi na bora ambayo yanaweza kukupa chochote kile unachokitaka kwenye maisha yako.

Hatua ya kuchukua;
Tengeneza orodha ya watu muhimu kwako unaohitaji kuwa na mahusiano nao ili warahisishe safari yako ya mafanikio.
Kisha kila siku weka juhudi za kutengeneza na kuboresha mahusiano na watu hao.
Unapohitaji kuongeza mtu mwingine muhimu kwenye orodha, fanya hivyo kisha endelea na mchakato wako wa kujenga na kuboresha mahusiano.

Tafakari;
Kwa chochote unachohitaji lakini unakwama, jiulize ni watu gani sahihi ambao hujawajua. Maana mkwamo mkubwa unatokana na kutokuwajua watu sahihi. Waliosema ongea na watu upate viatu walikuwa sahihi. Ni watu ndiyo wenye kila unachotaka. Jenga na boresha mahusiano yako na watu sahihi ili kupata unachotaka.

Kocha.