Rafiki yangu mpendwa,
Kila mmoja wetu kuna vitu ambavyo anavipenda sana kwenye maisha yake.
Vitu ambavyo hayupo tayari kuzuiwa na chochote kile katika kuvifanya au kuwa navyo.
Ni vitu hivyo ambavyo vinatoka ndani ya mioyo yetu kweli ndipo mafanikio yetu makubwa yamejificha.

Japo wengi huwa tunapuuzia vitu hivyo na kuhangaika na mengine, hilo limekuwa linachangia sana wengi kutokufanikiwa.

Hata kwenye kazi na biashara, kuna vitu ambavyo huwa tunavipenda kweli kutoka ndani ya mioyo yetu na kuwa tayari kuvifanya kwa namna yoyote ile. Hivyo ndivyo ambavyo tukivipa kipaumbele, tunakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa.

Lakini kupenda kufanya kitu haimaanishi kwamba hautakutana na changamoto mbalimbali.
Changamoto bado zitakuwa pale pale na kadiri unavyozitatua ndivyo unavyokaribisha nyingine kubwa zaidi.

Karibu kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kupata mafanikio tunayoyataka.
Hapa tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kupata ushauri na uzoefu wa kufanya biashara unayoipenda.

Kabla hatujapata ushauri wa hatua zipi za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

“Dr. Makirita, natamani sana kuanza kufanya biashara ya madini aina ya dhahabu. Changamoto inayonikabili ni mtaji wa uhakika pamoja na wapi pa kuanzia (connection). Naomba msaada, nifanyeje ili nifikie leno langu langu la kufanya biashara hii ambayo ninaipenda sana?” – Alfred M. M.

Kama alivyoeleza msomaji mwenzetu Alfred, kuna wengine pia ambao wanapenda kufanya biashara za aina fulani lakini wanakwamishwa na vikwazo mbalimbali.
Hapa unakwenda kujifunza hatua tano za kuchukua ili kuyavuka hayo;

Hatua ya kwanza; fanya kazi kujifunza.

Mtaji wa kwanza na muhimu unaohitaji kwenye biashara yoyote ni ujuzi na uzoefu.
Hivi unavipata kupitia kufanya kuliko njia nyingine yoyote.
Hivyo kwa biashara unayotaka kufanya, anza kwa kufanya kazi kwenye biashara ya aina hiyo ili kujifunza.

Hapa unatafuta kazi kwenye kampuni au taasisi inayojihusisha na kazi inayoendana na biashara unayotaka kufanya.
Hapo unapaswa kuwa tayari kwa kazi ya aina yoyote kwenye tasnia hiyo na kuwa tayari kulipwa kidogo.
Lengo lako hapa siyo malipo, bali kujifunza zaidi.

Na unapopata kazi ya aina hii, weka nguvu zako kubwa kujifunza kila kinachohusika.
Kwa sababu ukiwa ndani una fursa nyingi za kujifunza kuliko ukiwa nje.

Hatua ya pili; jifunze kwa ziada.

Kupata kazi inayoendana na biashara unayotaka kufanya ni hatua moja na muhimu.
Mwanzo utajifunza mengi, lakini baadaye utajikuta kwenye mazoea.
Utakuta mambo mengi yanafanyika kwa mazoea na hapo hupati tena fursa za kuendelea kujifunza.

Hapa ndipo unapohitaji kujifunza kwa makusudi na ziada ili ujenge ujuzi na uzoefu sahihi.
Jifunze kupitia usomaji wa vitabu na maarifa mengine, kisha jaribu yale mapya unayokuwa umejifunza.
Jifunze kwa kuendelea kuwa mdadisi na kuhoji kila unachokabiliana nacho.

Njaa na kiu yako ya kujifunza vinapaswa kuwa endelevu ili ujenge ujuzi na uzoefu mkubwa.
Usikubali kufanya tu kwa mazoea.

Hatua ya tatu; kusanya mtaji kidogo kidogo.

Mtaji mzuri wa kuanza biashara yoyote ile ni ule ambao umeukusanya mwenyewe.
Hiyo ni kwa sababu mwanzo wa kila biashara una changamoto kubwa, hivyo ni vyema kuingia kwenye hatari hiyo kwa fedha zako mwenyewe.

Wakati unafanya kazi kujifunza, endelea na zoezi la kukusanya mtaji.
Kuwa na akaunti maalumu ambayo unaweka akiba kutoka kwenye kila kipato unachoingiza.
Ukishaweka fedha huko isahau kabisa na usiiweke tena kwenye hesabu zako za matumizi.

Kwa kujipa muda na kuweka akiba ya mtaji bila kuacha, utaweza kujenga msingi wa mahali unapoweza kuanzia na kupiga hatua.

Hatua ya nne; tengeneza mtandao sahihi.

Unaowajua ni muhimu kuliko unachojua. Mtandao sahihi ni muhimu sana kwenye biashara.
Ni watu ndiyo watakaokupa fursa mbalimbali.
Ni watu ndiyo watakaokuwa wateja wako.

Hivyo wakati unajenga ujuzi na uzoefu, kazana pia kujenga mtandao sahihi.
Jua watu muhimu na wenye ushawishi kwenye biashara unayotaka kuingia kisha jenga nao mahusiano sahihi.

Na mahusiano mazuri yanajengwa kwa kutoa thamani kwa watu, siyo kwa kujipendekeza.
Ukishajua mtu unayemhitaji kwenye mtandao wako, angalia nini wanahitaji kisha wapatie.
Kwa kutoa thamani kwa wengine, unajiweka kwenye nafasi ya wao kukupa kile unachotaka pia.

Kujenga mtandao sahihi ni zoezi endelevu ambalo utaendelea nalo katika kipindi chote cha biashara.

Hatua ya tano; anza ukiwa bado kwenye kazi.

Baada ya kujifunza na kupata ujuzi na uzoefu wa kutosha, huku ukiwa umejenga mtandao mzuri, unapaswa kuanza kufanya biashara.
Unapaswa kuanza kufanya kidogo, huku ukiwa bado unaendelea na kazi unayofanya.

Anza biashara kidogo kidogo, kwa pale unapoweza kuanzia na kile unachoweza kuanza nacho.
Anza biashara hiyo ukiwa unaendelea na kazi yako, badala ya kuacha kazi ndiyo uende kufanya biashara.

Kwa kuanza biashara ukiwa bado una kazi nyingine unayoifanya, unaipa biashara nafasi ya kukua kabla hujaanza kuitegemea kama chanzo cha kipato.

Endelea kuikuza biashara yako ukiwa unaendelea na kazi mpaka pale itakapoweza kujiendesha yenyewe na kwa faida ndiyo uache kazi yako na kuweka nguvu zote kwenye biashara hiyo kuikuza zaidi.

Rasilimali muhimu;
Kuna rasilimali muhimu unapaswa kuwa nazo kama utachagua safari hii.
1. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kitakusaidia sana kukuza mtaji wako.
2. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA kitakusaidia kujenga mfumo sahihi wa kuiendesha.
3. Kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA kitakuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa unaendelea na kazi yako.
Kupata vitabu hivi wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa popote ulipo.

Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kujenga uzoefu na mtaji wa kufanya biashara unayoipenda.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.