2508; Kama Huna Cha Kufanya, Usifanye Chochote.
Kuna mambo mawili makubwa yanaendelea kwenye zama tunazoishi sasa.
Moja ni kila mtu amechoka kweli kweli, haijalishi amezalisha matokeo gani.
Mbili ni ubunifu na uvumbuzi umepungua sana.
Yote hayo yanasababishwa na tabia ya watu kukosa muda ambao hawana kitu cha kufanya.
Kwenye zama hizi, watu wana vitu vya kufanya muda wote ambao wapo macho.
Mtu anapopata dakika tano ambazo hana cha kufanya, anakimbilia kushika simu yake, anaingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kuperuzi.
Hilo linakuwa kazi kubwa kwake na inayomchosha.
Kama unataka kuwa tofauti na wengi, epuka sana hili.
Pale unapokuwa huna cha kufanya, usifanye chochote.
Wewe kaa tu kwenye huo muda ulionao mpaka uishe.
Kwa kufanya hivi unanufaika na mambo mawili makubwa.
La kwanza ni kupata mapumziko, pale unapokuwa hufanyi chochote, hutumii nguvu yoyote.
La pili ni kupata mawazo ya tofauti ambayo yanachochea ubunifu na uvumbuzi. Akili yako haiwezi kupata mawazo ya aina hiyo kama muda wote imetingwa na mambo yasiyo na tija.
Kuwa na muda ambao huna cha kufanya na kweli kutokufanya chochote inaweza kuonekana ni kupoteza muda. Lakini kuna manufaa makubwa kwa mtu anayefanya hivyo.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila siku yako, tenga muda ambao unakuwa huna kitu cha kufanya na kweli usifanye chochote kwenye muda huo.
Na pia inapotokea umepata muda ambao huna cha kufanya, labda kuna kitu unasubiri, usikimbilie kwenye simu na mitandao, kaa hapo bila ya kufanya chochote na utaweza kunufaika sana na hali hiyo.
Tafakari;
Akili iliyotingwa muda wote huwa haina nafasi ya kuleta mawazo ya tofauti, ya kibunifu na yanayoleta uvumbuzi mpya. Ipe akili yako muda ambao haina cha kufanya ili uweze kufanya makubwa.
Kocha.