Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha wewe ni mgeni hapa duniani.
Umetokea sayari ya mbali huko, ambapo chakula kikuu cha huko ni kula wadudu na mizizi ya miti.
Unafika kwenye hii sayari ya dunia na kuona mambo mengi ni tofuati na sayari uliyotoka.
Moja linalokushangaza sana ni hili.
Kuna watu wana mazao ya chakula, lakini badala ya kula mazao hayo, wao wanaenda kuyazika kwenye ardhi.
Unashangazwa sana na hilo tukio, maana watu hao wanaweza kuwa hawana kitu cha kula, halafu wanachukua chakula ambacho wangeweza kula na kwenda kufukia kwenye ardhi.
Kwa haraka haraka unaweza kuona huo ni ushirikina, au ujinga.
Unavutiwa kufuatilia zaidi hilo.
Siku inayofuata unatembelea walipofukia mazao hayo, huoni kinachoendelea.
Unaenda tena siku ya pili, ya tatu ya nne, hakuna kinachotokea.
Siku ya tano inanyesha mvua kubwa sana.
Na siku mbili baadaye unaona vitu vinaanza kuchomoza mahali yalipofukiwa mazao.

Unazidi kuvutiwa na hilo, unajiambia labda hawa watu kuna kitu wanajua. Unafuatilia hilo kwa muda, mbegu zinachipua, zinakua na kuzalisha mazao mengi zaidi.
Na hapo ndipo unaelewa kile wanachojua watu wa sayari ya dunia, kwamba kama unataka kupata mazao zaidi, lazima uwe tayari kuzika sehemu ya mazao kidogo.
Wengi wa tunaosoma hapa tumetokea familia ambazo zimewahi kujihusisha na kilimo au sisi wenyewe tunafanya kilimo moja kwa moja.
Kwa kipindi chote ambacho umekuwa kwenye kilimo, unajua kabisa bila ya shaka yoyote kwamba huwezi kupata mazao zaidi bila ya kuzika baadhi ya mazao.
Na unajua wakati mwingine unaweza kuzika mbegu na bado zisiote, hivyo kulazimika kuzika tena.
Hayo tunajua bila ya shaka yoyote.
Na ukishapanda mbegu, unajua kabisa ni muda gani wa kusubiri ndiyo zianze kuchipua.
Hupandi mbegu leo halafu kesho ukaenda kuanza kufukua kuona kama zinaota.
Ukishapanda unasubiri kwa muda sahihi wa mbegu husika kuweza kuchipua.
Somo hilo kubwa sana ambalo umejifunza kwenye kilimo, unalihitaji sana kwenye safari ya mafanikio.
Kwa sababu kwenye safari hiyo kuna msingi muhimu wa kupanda mbegu na muda wa kusubiri ndiyo ianze kuchipua.
Wengi wanapoianza safari ya mafanikio huwa na matarajio ya muda mfupi. Kwamba ndani ya muda mfupi watakuwa wamepata mafanikio makubwa.
Wakiona muda unaenda na hawafanikiwi kama walivyotaka, wanaona wamekosea njia, wanaenda kujaribu kitu kingine.
Hii haina tofauti na mtu anayepanda mbegu asubuhi halafu jioni anaenda kuzifukua kuangalia kama zimeota. Akiona hazijaota anafukua zote na kupanda mbegu nyingine.
Unajua kabisa mtu anayefanya hivyo hawezi kuvuna mazao yoyote.
Lakini mbona umekuwa unajifanyia hivyo wewe mwenyewe?
Umekuwa unavuruga safari yako ya mafanikio kwa sababu ya matarajio ambayo hayana uhalisia.
Watu wengi wameachana na malengo yao makubwa ndani ya muda mfupi kwa sababu wamekosa mtazamo sahihi wa nini kinahitajika ili kufikia malengo hayo.
Wanakata tamaa haraka na kuona malengo waliyojiwekea siyo sahihi, kumbe tatizo siyo malengo, bali matarajio yao.
Kwa kawaida huwa inachukua miaka miwili mpaka mitatu ya kuweka juhudi kubwa bila kuacha huku kukiwa hakuna matokeo yoyote yanayoonekana.
Yaani pamoja na kujituma sana kwa kipindi hicho chote cha miaka miwili, hakuna chochote unachoweza kuonyesha kama matokeo.
Hiyo ndiyo ninayoiita miaka miwili ya kuzika. Kipindi ambacho utaweka juhudi kubwa mno, lakini hakuna matokeo makubwa utakayokuwa unazalisha.
Lakini juhudi hizo zinakuwa hazijapotea, bali zinakuwa zimejenga msingi imara kabisa.
Kwani miaka mitano inayofuatia, juhudi unazoweka zinazalisha matokeo makubwa sana, mpaka watu kuona kama una bahati, maana siyo kwa mambo hayo mazuri yanayokuja kwako.
Ambacho watu hawawezi kuona ni ile miaka miwili ambayo uliizika, miaka miwili ambayo uliweka juhudi kubwa na hukuzalisha matokeo yoyote yale.
Dhana hii ya miaka miwili ya kuzika ndiyo inawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa wanaamini kwenye mchakato, hivyo hawahesabu kama muda unapotea, wao wanajua wanawekeza. Mtazamo huo unawawezesha kuvuka kipindi hicho na kufika kwenye kipindi kizuri na chenye mavuno makubwa.
Wanaoshindwa ndiyo wanaohangaika na matokeo, wakiona yanachelewa wanaachana na kitu hicho na kwenda kuanza kingine. Huko nako wanaona wanachelewa na kuacha.
Ndani ya muda wanajikuta wamejaribu vitu vingi, ila hakuna matokeo makubwa waliyozalisha.
Rafiki yangu mpendwa, wito wangu kwako ni huu, miaka miwili, miaka mitano na hata miaka kumi itapita tu. Iwe utafanya makubwa au madogo, muda hautasimama, utaendelea kwenda.
Hivyo basi, wewe kuwa na ndoto kubwa unazotaka kuzifikia kwenye maisha yako.
Jiwekee malengo ya kukufikisha kwenye ndoto hizo kubwa.
Weka mpango wa kutekeleza malengo yako.
Na kisha kuwa na mchakato unaoufanyia kazi kila siku.
Ukishakuwa na mchakato, huo ndiyo unapaswa kupambana nao kila siku.
Wewe wajibu wako ni kukaa kwenye mchakato.
Pambana na mchakato na usilazimishe majibu.
Kwani mchakato sahihi huleta majibu sahihi kwa wakati wake.
Usiangalie ni muda kiasi gani umepita, wewe angalia ni namna gani unatekeleza mchakato wako kila siku.
Pambana na mchakato bila ya kujali muda na utaweza kuzalisha matokeo makubwa na kuzifikia ndoto kubwa ulizonazo.
Iendee safari yako ya mafanikio kama mkulima, kwa kupambana na mchakato wako na kuyaacha matokeo yaje kwa wakati wake.
Je ni ndoto zipi kubwa ulizonazo?
Ni malengo gani unayo katika kuzifikia?
Ipi mipango yako katika kufikia malengo yako?
Na upi mchakato wako wa kufanyia kazi kila siku?
Kama hujachambua safari yako kwa namna hiyo, itakuwa vigumu sana kwako kufika unakotaka.
Hakikisha umepata na kusoma kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO ili ujijengee misingi sahihi ya kukuwezesha kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kitabu hiki kinakujengea mtazamo sahihi utakaokuweka kwenye mchakati sahihi wa mafanikio ili usikatishwe tamaa na matokeo unayokuwa unayapata.
Wasiliana na 0752 977 170 ili kupata nakala yako ya kitabu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.somavitabu.co.tz