#SheriaYaLeo (13/366); Bobea kwenye vitu vidogo.

Pale unapokuwa umekabiliwa na mapungufu badala ya uimara, huu ndiyo mkakati unaopaswa kufanyia kazi; puuza udhaifu wako na kataa ushawishi wa kutaka kuwa kama wengine.

Badala yake weka juhudi zako zote kwenye vitu vidogo vidogo ambavyo uko vizuri katika kuvifanya.
Usihangaike na mambo makubwa katika wakati huo, wewe chagua vitu vidogo ambavyo uko vizuri na hakikisha unavibobea kabisa.
Hilo litakujengea kujiamini na huo kuwa msingi ambao unaweza kuutumia kukua zaidi.

Kuendelea kwa namna hiyo, hatua kwa hatua utaweza kufika kwenye kusudi na wajibu wa maisha yako.
Siyo mara zote utaweza kujua kusudi na wajibu wa maisha yako kupitia malengo makubwa.
Unaweza kujua kupitia madhaifu uliyonayo yanayokusukuma kuweka mkazo kwenye vitu vidogo vidogo ambavyo uko vizuri.
Kwa kufanyia kazi vitu hivyo vidogo unajifunza nidhamu muhimu ambayo itakuwezesha kufanya makubwa zaidi.
Ujuzi wako utakua kwa kuanzia kwenye vitu hivyo vidogo na kwenda kwenye vikubwa zaidi.

Usiwaonee wivu wale wanaoonekana kuwa na vipaji kuliko wewe. Mara nyingi vipaji hivyo huwa laana kwao kwa sababu huwa hawajifunzi umuhimu wa nidhamu. Hilo huja kuwagharimu sana baadaye.

Kwa kila kikwazo unachokutana nacho kwenye maisha, wewe weka mkazo kwenye vitu vidogo vidogo ambavyo upo vizuri. Anzia hapo kujenga msingi utakaokuwezesha kukua zaidi.

Sheria ya leo; Unapokuwa njia panda, weka mkazo kwenye vitu unavyojua kuvifanya vizuri. Jenga msingi na kua kuanzia hapo.