2523; Tatizo unataka kusikia unachotaka.

Zoezi la kutoa na kupokea ushauri limekuwa zoezi lisilo na manufaa kwa wengi wanaoshiriki.

Hiyo ni kwa sababu watu wengi wanaoomba ushauri, siyo kama wanataka ushauri kweli, ila wanataka wajue kama maamuzi waliyofanya ni sahihi.

Yaani ndani yao wanakuwa tayari wameshafanya maamuzi, ila wanaomba ushauri ili kuona kama wengine nao wangefanya maanuzi kama yake.

Kinachotokea ni mtu kusema amepewa ushauri mzuri pale anachoshauriwa kinaendana na maamuzi anayotaka.
Au mtu kusema amepewa ushauri mbaya pale anachoshauriwa kinapingana na maamuzi anayotaka.

Hili pia limekuwa kikwazo kwenye kujifunza, watu hawajifunzi kwa sababu hawasikilizi au kutuatilia kile kinachofundishwa, bali wanataka kusikia kile wanachotaka kusikia.
Hivyo kama wanachotaka kusikia hakisemwi, basi wanaona yanayosemwa siyo sahihi.

Kila siku na kwenye kila hali unakutana na fursa nyingi sana za kuweza kujifunza na kuchukua hatua za tofauti na kupata matokeo makubwa.
Lakini huzioni fursa hizo kwa sababu umetingwa na kutafuta vitu ambavyo unataka kuona na kusikia wewe.
Unapoteza vitu vizuri kwa kuhangaika na vitu vya kufikirika.
Hapo ndipo unapokwama.

Hatua ya kuchukua;
Kuanzia sasa, weka umakini wako kwenye kila kinachosemwa au kinachoendelea, angalia kila kitu kama kilivyo na siyo kutaka kiwe vile unavyotaka wewe.
Ukiondoa huo upendeleo wako na kuweka umakini wako wote utajifunza mengi na kuweza kuzitumia fursa mbalimbali kupiga hatua.

Tafakari;
Kutaka kusikia unachotaka kusikia na kuona unachotaka kuona ndiyo adui mkubwa wa mafanikio yako. Maana unazikosa fursa nzuri za kujifunza na kuchukua hatua ili kupata matokeo ya tofauti.

Kocha.