2524; Pesa ziko wapi?

Wahenga walisema, mali bila daftari, hutumika bila habari.
Kama hutunzi vizuri kumbukumbu zako za kila senti inayoingia na kutoka, hutajua pesa zako zinapotelea wapi.
Utaona tu umeshika pesa nyingi, lakini hujui zimeenda wapi.

Na hapo ndipo wengi huamini kuna chuma ulete, hali ya ushirikina ambapo fedha zinachukuliwa bila mtu kujua.
Wanachoita watu chuma ulete ni uzembe ambao wanakuwa nao kwenye kutunza kumbukumbu zao za kifedha.

Kuna sababu kwa nini chuma ulete hawaendi benki kujichotea mapesa yaliyopo na kuhangaika na vijisenti vya wenye biashara ndogo mitaani.
Kwa sababu benki hakuna uzembe, kila kitu kinawekwa kwenye kumbukumbu.
Lakini kwenye biashara ndogo za mitaani, watu huona kuweka kumbukumbu ni kujipotezea muda, hivyo wanapoteza fedha nyingi na kusingizia chuma ulete.

Wahenga pia walisema, penye uzia penyeza rupia.
Inapojitokeza fursa yoyote ile, watu huitumia.
Na hili pia linahusika kwenye fedha zako, kama kuna nafasi ya watu kujipatia fedha zako kirahisi, iwe ni kwa kuomba au kuiba, watafanya hivyo.

Kama huna udhibiti mzuri wa fedha zako, kama kuna mianya ambayo watu wanaweza kujipatia watakavyo, jua wataitumia.
Na kwa kuwa huwezi vizuri kumbukumbu za fedha zako, hutajua chochote kinachoendelea.

Hatua ya kuchukua;
Weka kumbukumbu za kila senti inayoingia na kutoka. Hakikisha unajua kwa kina kila pesa yako iko wapi.
Na ondoa kila mwanya wa watu kuzipata pesa zako kwa manufaa yao huku wewe ukizipoteza.

Tafakari;
Kama una uvivu kiasi cha kushindwa kudhibiti pesa zako, unastahili kuzipoteza. Hivyo usipige kelele pesa ziko wapi wakati unazipoteza wewe mwenyewe.

Kocha.