2530; Mnyoo Mjinga.

Kwenye baiolojia kuna dhana kwamba mnyoo (parasite) mwenye akili anahakikisha kiumbe anayemtegemea hafi.
Hivyo hata kama anamnyonya virutubisho mbalimbali, anahakikisha hachukui kila kitu mpaka kupelekea afe.

Hiyo ni kwa sababu kama kiumbe ambaye mnyoo anamtegemea atakufa, basi na yeye atakufa pia.
Hivyo tunaweza kusema mnyoo ambao unamuua mwenyeji wake, ni mnyoo mjinga.

Sawa, sasa hapa hatuzungumzii minyoo, bali sisi binadamu.
Huwa tunategemeana kwa namna fulani ili maisha yaweze kwenda.
Mwajiri anamtegemea mfanyakazi huku mfanyakazi akimtegemea mwajiri.
Kadhalika mfanyabiashara anamtegemea mteja huku mteja akimtegemea mfanyabiashara.

Hakuna kitu chochote unachoweza kufanya hapa duniani bila ya kutegemea watu wengine.
Na hapo ndipo unapopaswa kuchagua ni aina gani ya watu wa kushirikiana nao au kuwategemea kwa namna mbalimbali.

Hapa ndipo dhana ya mnyoo itaweza kukusaidia sana.
Kama mtu yupo tayari wewe ufe au upoteze ili tu yeye apate, huyo siyo mtu sahihi wa kushirikiana naye au kumtegemea. Kwa sababu fursa itakapojitokeza, hatasita kukupoteza au kukuharibia ili tu yeye apate.

Mfano kama umeajiri mfanyakazi kwenye biashara yako, kisha akawa mwizi ambaye anaiba kwenye biashara, huyo ni mnyoo mjinga. Maana anachofanya kinaweza kuua biashara na biashara ikifa hana tena kazi.

Zijue tabia za watu mapema kisha achana nao kama hawafai. Usijidanganye kwamba utaweza kuwadhibiti au kuwabadilisha. Wanaweza kuigiza kwa muda, ila kuna siku watapata upenyo na watakuonyesha kweli madhara yao.

Hatua ya kuchukua;
Usiwe mnyoo mjinga kwa kudhuru wale unaowategemea.
Na pia gundua minyoo wajinga kwenye maisha yako na wafute mara moja, usiwape nafasi maana kwa ujinga wai watakudhuru sana.

Tafakari;
Huwa kuna usemi maarufu kwamba usijisaidie pale unapokula. Ni kauli fupi na yenye ujumbe mzito, lakini watu wanaichukulia poa. Wewe izingatie sana.

Kocha.