Rafiki yangu mpendwa,
Vipi kama leo nitakuambia kuna mambo mawili unayoweza kufanya kila siku na ukaongezea miaka 20 kwenye maisha yako?

Yaani kama ilikuwa uishi miaka 60, basi kwa kufanya kitu hicho utaweza kuishi miaka 80. Na kama ilikuwa uishi miaka 80 basi utaishi miaka zaidi ya 100.

Na kama huwezi kukadiria ni umri gani ungeishi, basi kwa kufanya mambo hayo mawili kila siku utaishi miaka zaidi ya 100.

Ndiyo, kwa sehemu kubwa sana, utaweza kuishi miaka mingi zaidi kwenye maisha yako, ukiondoa hatari zinazoweza kuyakatisha kama ajali na vingine.

Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa tunatafuta siri za kuweza kuongeza umri wetu wa kuishi.
Pamoja na maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya, umri wa watu kuishi umeongezeka, lakini bado una ukomo mkubwa.

Watu wengi sasa wanaishi mpaka miaka 80, lakini ni wachache wanaoishi miaka zaidi ya 100.
Katika hao wachache wanaoishi miaka zaidi ya 100, kuna tafiti mbalimbali zimefanywa na zimeonyesha kuna utofauti kati ya wale wanaoishi miaka mingi na wanaoishi miaka michache.

Ni sehemu ya tafiti hizo ndiyo tunakwenda kujifunza kitu kimoja unachoweza kufanya kila siku na kikaongeza miaka yako ya kuishi hapa duniani.

David Sinclair, Profesa wa Baiolojia wa chuo kikuu cha Harvard, ambaye pia ni mwandishi wa kitabu kinachoitwa Lifespan, anatuambia kwamba kutatua changamoto ya kuzeeka ni jambo rahisi.
Kwenye kitabu hicho anaeleza kutatua tatizo la uzee ni rahisi kuliko kutatua tatizo la saratani.

Kuna dhana mbalimbali zinazoeleza kwa nini binadamu huwa tunazeeka.
Na moja kubwa ni kwamba kadiri mtu anavyoishi miaka mingi, ndivyo seli za mwili wake zinavyogawanyika mara nyingi.
Katika kugawanyika huko kwa seli, makosa mbalimbali yanajitokeza na hapo seli mpya zinakuwa dhaifu kuliko za awali.

Kwa lugha nyepesi, mwili unachoka kama ambavyo gari linachoka na kuharibika baada ya kutumiwa kwa muda mrefu.

Tunajua nini huwa tunafanya kwenye magari ili yasichoke haraka, kwa kuyafanyia ‘service’ mara kwa mara.
Ndiyo, kadiri gari inavyofanyiwa matengenezo ndivyo inavyodumu kwa muda mrefu zaidi.

Kwa dhana hiyo hiyo, miili yetu ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara itaweza kudumu kwa muda mrefu bila ya kuchoka kunakotokana na mgawanyiko wa seli.

Swali ni je mwili unawezaje kujitengeneza mara kwa mara ili kuepuka uzee?
Hilo ndiyo Sinclair anajibu baada ya kufanya na kukusanya tafiti mbalimbali za kibaiolojia.

Kupitia tafiti hizo, Sinclair amegundua kwamba mwili tayari unao mfumo wake wa kujitengeneza wengewe, yaani kurekebisha seli za mwili ambazo zimekuwa na makosa kwenye kugawanyika.
Mfumo huo unatumia protini zinazoitwa sirtuins. Protini hizo zinapopata taarifa kuhusu seli ambazo hazipo sawa, zinafanya kazi ya kurekebisha hilo kwa kuondoa seli hizo.

Tafiti zilizofanywa kwa wanyama mbalimbali kama panya, zinaonyesha wanyama walioongezewa protini hiyo ya sirtuins waliishi kwa umri mrefu zaidi, asilimia 30 zaidi ya umri uliozoeleka.
Kwa matokeo ya tafiti hizi, baadhi ya watu wameanza kufanya majaribio kwa binadamu, kuongeza protini hizo ili mwili uweze kujitengeneza wenyewe.

Lakini hizo ni tafiti kubwa ambazo zinahitaji gharama na vibali mbalimbali kufanyika na siyo wote wanaweza kujaribu.
Je kuna njia mbadala ya kuongeza protini hizo au kuzichochea kufanya kazi yake ili mwili uweze kujirekebisha wenyewe?

Jibu ni ndiyo, kutokana na tafiti mbalimbali, Sinclair ameshirikisha njia nyingine mbadala za kuchochea protini ya sirtuins.
Alichogundua ni kwamba wakati ambao mwili unapitia hali ngumu, kama ya njaa au hali ngumu, sirtuins huwa inazalishwa kwa wingi na kufanya kazi ya kurekebisha seli mbalimbali kwenye mwili, kitu kinachozuia mtu asizeeke haraka.

Na hapo kuna njia mbili za kuuweka mwili kwenye hali ambayo itachochea zaidi sirtuins zifanye kazi yake.

Njia ya kwanza ni kupunguza kula.

Mwili unapokuwa na njaa, sirtuins zinachochewa zaidi na kufanya kazi ya marekebisho kwenye seli zote za mwili ambazo hazipo sawa.
Unaweza kufikia hili kwa namna mbili;

Moja ni kula kiasi kidogo sana cha chakula. Hapa unakula kidogo mno na mara moja au mara mbili kwa siku.
Huli mpaka ukashiba, bali unakula kidogo tu kuupa mwili nguvu ya kuendesha maisha. Kwa kipindi kirefu unakaa na njaa na hapo mwili unachochea zaidi sirtuins zifanye kazi yake.

Mbili ni kufunga, hapa unaweza kufunga kwa vipindi fulani kwenye siku yako, au kufunga kwa siku kadhaa kwenye wiki au mwezi na kadhalika. Kadiri unavyofunga ndivyo unavyouweka mwili kwenye hali ya kujifanyia matengenezo zaidi.

Kwa kifupi hapa tunaweza kusema; KAMA UNATAKA KUISHI MIAKA MINGI, PUNGUZA KULA.
Na wapo watu wengi ambao wameweza kuishi miaka zaidi ya 100 kwa kudhibiti sana ulaji wao.

Njia ya pili ni kuuweka mwili kwenye hali ngumu ambapi sirtuins zitachochewa na kufanya marekebisho. Hali ngumu unazoweza kuuweka mwili ni kama mazoezi makali, kuoga maji ya baridi sana au kukaa kwenye hali ya joto kali.
Yote hayo yanaufanya mwili uone unapitia hali ngumu kitu kinachochochea protini ya sirtuins kufanya marekebisho.

Rafiki, hizi zote ni tafiti ambazo bado zinaendelea kufanyika na kupitia watu waliojaribu haya huko nyuma na wanaoendelea kujaribu sasa, tutaendelea kupata matokeo ambayo yataonyesha kama kweli ni njia bora na zinazofanya kazi.

Lakini kwa kuwa hakuna unachopoteza kwa kupunguza kula na kuongeza kufanya mazoezi, basi nishauri ufanye vitu hivyo, kwani vimethibitishwa kuimarisha afya yako na pia vinaweza kuongeza umri wako wa kuishi.

Punguza sana ulaji wako, kula kidogo sana na mara chache mno kwa siku. Hakikisha kwenye kipindi kirefu cha siku unasikia njaa kabisa, hapo ndipo mwili unapofanya kazi ya kujitengeneza.
Pia unaweza kuchagua siku ambazo utakuwa unafunga kutokula kabisa kwenye wiki yako.

Na muhimu kabisa, fanya mazoezi makali mara kwa mara, angalau nusu saa ya mazoezi makali kila siku inauweka mwili kwenye hali ya ugumu unaochochea maboresho kufanyika.

Kudhibiti ulaji na kufanya mazoezi ni vitu ambavyo tayari vipo ndani ya uwezo wako, vifanyie kazi sasa kuboresha afya yako na kuongeza umri wa maisha yako.

Rafiki, hivi unajua mwili wako una uwezo mkubwa kuliko unavyojua wewe?
Unajua ukiweza kutumia uwezo huo vizuri utafanya makubwa sana hapa duniani?
Kama bado hujajua hilo kwa kina, pata na usome kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA.
Kitabu hiki kitakuonyesha nguvu kubwa ambayo tayari ipo ndani yako na jinsi unavyoweza kuitumia kufanya makubwa.
Kupata kitabu hiki wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.

Makala hii imeandikwa na rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
Ambaye ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.