2531; Usijipe umuhimu usiokuwa nao.
Ndiyo, wewe ni mtu muhimu sana kwako, mtu wa kipekee, mwenye uwezo mkubwa mno.
Hayo yote yako ndani yako tayari.
Lakini unashindwa kuyatumia kwa sababu unajipa umuhimu kupitiliza, umuhimu usiokuwa nao.
Pale unapodhani kwamba dunia inapaswa kwenda kwa matakwa yako wewe unajidanganya sana.
Kwa sababu utakata tamaa pale dunia inapokwenda tofauti na matarajio yako.
Pale unapodhani kila mtu anakuangalia wewe unajizuia kufanya makubwa.
Kwa sababu unaona ukijaribu kitu na ukashindwa basi dunia nzima itakucheka.
Ndiyo, wewe ni muhimu kwako mwenyewe. Lakini nje ya hapo, huna ule umuhimu ambao unajipa sana.
Mfano ikitokea umekufa leo, dunia haitasimama, mambk yataendelea kwenda kama kawaida.
Hata watu unaodhani wanakutegemea sana, unaoona bila wewe hawawezi kwenda, amini usiamini, ukifa leo, baada ya siku chache tu wataendelea kwenda kama kawaida.
Kujua hili haipaswi kutukatisha tamaa, badala yake kutuweka huru kuyaishi maisha yetu.
Na pale tunapokuwa huru kuyaishi maisha yetu ndiyo tunajiweka kwenye nafasi ya kufanya mambo makubwa.
Kwa sababu hatujali sana kuhusu wengine, tunakuwa huru kufanya yale yaliyo ndani yetu na hilo ndiyo linalotutofautisha na wengine.
Hatua ya kuchukua;
Jikumbushe kwamba nje yako huna umuhimu ambao umekuwa unajipa, hivyo kuwa huru kuyaishi maisha yako. Jikumbushe wengi ulioona ni muhimu sana hapa duniani, lakini baada kuondoka kwao dunia haijasimama. Jua hiyo ndiyo hatima yako pia, na kuwa huru kuishi kwa wakati huu ulionao.
Tafakari;
Dunia imekuwepo kwa miaka mingi kabla yako na itaendelea kuwepo kwa miaka mingi baada yako. Huidai dunia chochote, bali dunia ndiyo inakudai wewe. Acha kujipa umuhimu usiokuwa nao, kuwa mnyenyekevu na ishi maisha yako.
Kocha.