#SheriaYaLeo (35/366); Thamini kujifunza kuliko mengine yote.

Kadiri unavyopiga hatua kwenye maisha yako, utasukumwa kutafuta fursa zinazokuingizia kipato kikubwa zaidi ili kuweza kuendana na hali ya maisha.
Hilo litakusukuma kutafuta kazi au biashara ambayo inakulipa vizuri zaidi.

Kwa bahati mbaya sana, unapopata kile kinacholipa zaidi, huwa hakina fursa za kujifunza ujuzi na uzoefu unaokuwa na thamani kubwa kwako kwa siku zijazo.
Hivyo muda unaotumia kukimbizana na kipato zaidi, ni muda ambao hutumii kujifunza.

Hata kama utapata fursa hizo zinazokupa kipato kizuri kwa sasa, baadaye hilo linakuja kukugharimu sana. Kwani unafika wakati ambapo huna ujuzi na uzoefu wenye thamani na hivyo kukosa fursa nzuri na kubwa zaidi.

Jua fedha hazina mwisho na kadiri unavyojifunza ndivyo unavyotengeneza fursa za kutengeneza kipato kikubwa zaidi baadaye.
Hivyo kipaumbele chako cha kwanza kwenye kuchagua fursa ni kuangalia nini unakwenda kujifunza. Ujuzi na uzoefu gani ambao utaondoka nao kwenye kitu hicho na ukawa wa thamani kubwa zaidi kwako.

Chagua watu ambao utajifunza kwao, hata kama ni kwa kuwafanyia kazi bure. Kwani kuwa karibu nao utajifunza vitu vingi vya ndani ambavyo siyo rahisi mtu akufundishe.

Usifanganyike na fedha za haraka ukashindwa kujijengea ujuzi na uzoefu wenye manufaa kwako kwa baadaye.

Sheria ya leo; Kipaumbele cha kwanza kwako kwenye fursa yoyote ile kinapaswa kuwa ni nini unajifunza ambacho kinakufanya kuwa bora zaidi. Tumia kigezo hicho kuchagua fursa sahihi kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu