2533; Madhara huonekana baadaye.

Kwenye safari ya mafanikio na maisha kwa ujumla huwa kuna njia mbili.
Ya kwanza ni njia ndefu, ambayo pia ndiyo njia sahihi. Ila njia hiyo inahitaji muda na juhudi kubwa ili kuweza kufika unakotaka.

Ya pili ni njia fupi na ya mkato, ambayo pia siyo njia sahihi. Ni njia isiyohitaji muda wala juhudi katika kufika unakotaka.

Njia za mkato huwa zinatangazwa na kukimbiliwa na wengi. Wote wanaopita kwenye njia hizo hujiona ni wajanja kuliko wale wanaopita njia ndefu. Na kwa haraka haraka wanaweza kujiona wananufaika kuliko wengine.

Ni baada ya muda mrefu ndiyo mambo yanajidhihirisha wazi. Njia za mkato zinakuwa zimezalisha madhara makubwa kuliko njia ndefu.

Ni wakati wa ujenzi ambapo mtu hatumii vipimo sahihi anapojisifu kwamba ametumia gharama ndogo. Ni mpaka baadaye jengo linapoharibika haraka ndiyo madhara yanaonekana.

Ni wakati wa ujana ambapo mtu anakimbilia kufanya chochote kinachoingiza fedha na kujisifu anaijua fedha.
Ni mpaka baadaye anapokuja kugundua umri umekwenda na hajajijengea ujuzi wowote wenye manufaa kwake.

Ni pale mtu anapoona hana muda wa kujifunza kupitia usomaji wa vitabu, kwa sababu ametingwa sana na yale anayofanya.
Ni mpaka baadaye ndiyo anagundua amekwama, hajafikia mafanikio makubwa ambayo yako ndani ya uwezo wake.

Hatua za kuchukua;
Jikumbushe kwenye maisha yako ni mara ngapi ulishawishika kutumia njia za mkato ila baadaye zikaja kuwa na madhara kwako?
Kuanzia sasa, kila unapokutana na njia ya mkato na njia ndefu, pita njia ndefu.
Ndiyo utachelewa na kutumia nguvu sana, lakini pia utafika kwa uhakika na hutatengeneza madhara yoyote.

Tafakari;
Bila ya kuangalia madhara ya muda mrefu, kila kitu huonekana kuwa kizuri ndani ya muda mfupi. Wewe usiwe wa kuangalia kwenye muda mfupi, bali angalia muda mrefu ujao na fanya maamuzi sahihi.

Kocha.