2534; Kazi haikwepeki, inaweza kuhamishwa.
Kazi haiwezi kukwepeka, ila inaweza kuhamishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Mwandishi mmoja amewahi kusema kama umeweza kusoma kitu kwa urahisi, jua mwandishi ameweka kazi kubwa kwenye kuandika.
Na kama kitu ni kigumu kusoma, jua mwandishi hajaweka kazi.
Maana yake ni rahisi, uandishi unahitaji kazi. Kama mwandishi ataweka kazi, msomaji hatahitaji kazi kubwa kwenye kusoma.
Lakini kama mwandishi atakwepa kazi, atakuwa ameihamishia kwa msomaji, ambaye atasoma kwa shida.
Hilo haliishii tu kwenye uandishi, bali linagusa kila eneo la maisha.
Kama anayepaswa kufanya kazi hutafanya kazi yake vizuri, atakuwa ameisukuma kazi hiyo kwa wale wanaokwenda kuitumia.
Kama mtu hatafanya kazi yake vizuri na kwa umakini, atakuwa ameihamishia kwa wale anaowalenga, ambao itakuwa vigumu kwao kutumia kazi hiyo.
Mwalimu ambaye hafanyi kazi yake ya kufundisha vizuri, anawapa wanafunzi kazi kubwa zaidi kwenye kujifunza.
Daktari ambaye hafanyi kazi yake ya kutibu vizuri, anawapa wagonjwa wake kazi zaidi kwa kukaa na maradhi muda mrefu.
Mfanyabiashara ambaye hafanyi kazi yake vizuri, anawapa kazi zaidi wateja wake kuhangaika na vitu visivyo sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jiulize kazi yako kuu ni ipi na uifanye vizuri ili kuepuka kuhamishia kazi hiyo kwa wengine.
Hakikisha unawarahisishia sana wale unaowalenga kwenye kile unachofanya.
Tafakari;
Usijidanganye umekwepa kazi au kupata njia ya mkato ya kupunguza kazi, jua umehamisha kazi hiyo kwenda kwa watu wengine. Na kwa kuwa watu hawapendi kazi, watakukimbia pale wewe unapokuwa unakwepa kazi na kuwapa wao kazi zaidi.
Kocha.