2536; Makubaliano ya kuridhishana.

Kwenye maisha na shughuli mbalimbali huwa tunakutana na hali za kutokukubaliana kwenye mambo mbalimbali.

Kutokana na uelewa, imani na mazoea tofauti ambayo watu wanayo, kwenye jambo moja watu wanaweza kuwa na mtazamo au maoni tofauti.

Kila mtu ataona upande wake ndiyo sahihi zaidi na kuamini upande mwingine ndiyo unaokosea.

Katika kuvuka hili na kuweza kushirikiana, watu huweza kukubaliana ili kuridhishana, hapa wanakuja na kitu cha katikati ambacho kinawaridhisha wote.

Kwa bahati mbaya sana kitu hicho cha kati hakimridhishi yeyote kwa sababu mara nyingi kinakuwa siyo ukweli wenyewe.

Kama mtu mmoja anasema A ndiyo sahihi na mwingine anasema C ndiyo sahihi, kama watakubaliaba ili kutidhishana na kuchagua B kuwa ndiyo sahihi, wanaishia kutoridhika.
Wote hawapati kilicho sahihi na hivyo kutokunufaika.

Jambo muhimu kabisa siyo kuridhishana, bali kuujua ukweli.
Na kama upande wa pili hautaki kujua ukweli, ni bora uuache na kile ambacho wanaamini kuliko kutengeneza makubaliano mapya kwa lengo la kuridhishana.

Hatua ya kuchukua;
Kumbuka ni mara ngapi umekubaliana mambo na wengine ili tu kuwaridhisha, lakini mwisho wa siku wao hawakuridhika na wewe pia hukuridhika?
Mara zote simamia kwenye ukweli, mkubaliane kwenye ukweli na siyo kwenye kuridhishana.
Ukweli haubembelezi, lakini pia haubadiliki. Kusimama kwenye ukweli ni kusimama kwenye upande sahihi.

Tafakari;
Ukweli ni mmoja na haujali sana kuhusu yeyote. Njia yoyote ambayo mtu atajaribu kupata makubaliano nje ya ukweli ni kujidanganya tu.

Kocha.