Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Four Thousand Weeks : Time Management for Mortals kilichoandikwa na Oliver Burkeman.

⭐UTANGULIZI; WOTE TUTAKUFA.

Maisha yetu sisi binadamu ni mafupi sana. Jamii ya binadamu tumekuwa hapa duniani kwa takribani miaka laki 2. Na wanasayansi wanakadiria kwamba jamii ya binadamu itaendelea kuwa hapa duniani kwa miaka mingine bilioni moja ijayo.
Hizo ni takwimu kwa jamii nzima ya binadamu, lakini kwa mtu mmoja mmoja, muda ni mfupi sana.

Kwa wastani mtu anaishi miaka 80, kwa wachache wenye nidhamu kubwa kiafya wanaweza kwenda mpaka miaka 100.
Kwa mwaka ambao una wastani wa wiki 52, miaka 80 ni kama wiki elfu nnne na kidogo.  Na kwa miaka mia moja ni wiki elfu tano na kidogo.
Hivyo kitabu hiki kimeandikwa kwa dhana kwamba kwa wastani, kila binadamu anapata wiki elfu 4 tu za kuishi hapa duniani.

Sasa hebu yaangalie maisha kwa upande huo, kwamba una wiki elfu 4 pekee, unaona jinsi maisha yalivyo mafupi?
Ni katika wiki hizo elfu 4 ndiyo unakazana kufanya yote unayotaka kufanya.
Na kama unasoma hapa, hesabu yako soyo elfu 4 tena, huenda ni chini ya elfu 3. Kwa sababu kama una miaka zaidi ua 20, umeshatumia wiki elfu moja, kama una miaka zaidi ya 40 umeshatumia wiki elfu 2.

Kwa kuangalia muda hivi, tunajionea jinsi ambavyo muda wetu hapa duniani ni mfupi na hivyo kupaswa kuutumia vizuri kama tunataka kuwa na maisha ya tofauti.

✔Tatizo la vitabu vingi vya usimamizi wa muda.

Kuna vitabu vingi sana ambavyo vimeandikwa kuhusu usimamizi na matumizi ya muda (time management).
Vitabu hivyo vinafundisha mbinu mbalimbali kwa watu kuweza kutumia muda wao vizuri na kufanya makubwa.

Lakini vitabu hivyo vina kosa moja kubwa, kufundisha jinsi ya kufanya mambo mengi zaidi kwenye muda ambao ni mfupi.
Kwa sababu mambo ya kufanya yanaongezeka, huku muda ukiwa ni ule ule, vitabu hivyo vimekuwa vinawafundisha watu jinsi wanavyoweza kufanya nambo mengi zaidi kwenye muda mfupi walionao.

Matokeo yake ni kama kuzima moto kwa petroli, kwani mtu anapokazana kufanya mengi ndani ya muda mfupi, ndivyo mengi zaidi ya kufanya yanavyoongezeka.

Kwa kifupi ni kwamba, hakuna mwisho wa mambo ya kufanya, kadiri unavyofanya mengi, ndivyo mengi zaidi ya kufanya yanavyojitokeza.
Hivyo badala ya mtu kuwa huru kadiri anavyofanya zaidi, anakuwa anajichimbia kaburi kwa kuwa na mengi zaidi ya kufanya.

Miaka ya 1930 aliyekuwa mchumi maarufu John Maynard Keynes alieleza kwamba ndani ya karne moja, teknolojia itakua imekuwa sana kiasi kwamba watu hawatahitajika kufanya kazi zaidi ya masaa 15 kwa wiki.
Watu watakuwa na muda mwingi ambapo hawahitajiki kufanya kazi na hivyo maisha kuwa bora.

Kwa bahati mbaya sana tunakamilisha huo muongo, huku teknolojia ikiwa imekua sana kiasi cha kurahisisha kazi, lakini hatuna muda kabisa.
Badala ya masaa ya kufanya kazi kupungua, ndiyo yameongezeka mara dufu.
Wakati kipindi cha nyuma watu walikuwa wanafanya kazi kwa masaa 40 tu kwa siku, au muda wa mchana tu, sasa watu wanafanya kazi muda mara mbili zaidi.
Watu wanafanya kazi zaidi ya masaa 80 kwa siki na wakati mwingine usiku na mchana. Na bado wanajiona hawajakamilisha yale muhimu.

Hivyo ushauri wa matumizi na usimamizi wa muda kwa kufanya zaidi, siyo tu kamba haupo sahihi, bali pia umekuwa na madhara makubwa. Kwani kadiri mtu anavyofanya zaidi, ndivyo vya kufanya vinaongezeka zaidi.

✔Kukamilisha visivyo sahihi.

Kila siku huwa inaanza na kuisha na kila mtu anakuwa amechoka mwisho wa siku kuliko mwanzo wa siku.
Kila mtu kuna mambo anakamilisha au anajaribu kukamilisha kwenye siku yake, lakini je hayo anayokamilisha yanamfikisha wapi?

Kwa bahati mbaya sana, mambo ambayo watu wanajitesa nayo, mambo ambayo yanawachosha katika kukamilisha ni mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye maisha yao.

Ndiyo watu wanakuwa bize,  ndiyo wanafanya mengi, lakini hayana mchango wowote wenye tija kwao.

Ukuaji wa teknolojia, ambao ulitegemewa upunguze muda wa watu kufanya kazi, umekuwa kinyuma, umeongeza zaidi muda huo.
Matumizi ya mtandao wa intaneti, mitandao ya kijamii, barua pepe na mikutano ya video imefanya kusiwe na mpaka kati ya kazi na maisha.

Hilo limepelekea watu kuwa wanafanya kazi muda wote, kitu ambacho kinawaletea uchoshi (burn out).
Hili linasababisha ufanisi wa watu kushuka, licha ya kuonekana watu wanajituma sana, hakuna wanachokamilisha.

Lakini pia ubize umekuwa ni kama sifa kwenye zama hizi. Watu wanaoonekana kuwa bize wakati wote ndiyo watu wanaoonekana wanafanya kazi sana, wakati matokeo ni tofauti kabisa.

✔Utofauti wa kitabu hiki.

Tofauti na vitabu vingine vya usimamizi na matumizi ya muda, kitabu hiki hakijaribu kuficha tatizo.
Bali kinaliweka tatizo wazi kabisa, kwamba muda wetu hapa duniani ni mfupi na haijalishi tutajaribu kufanya mambo mengi kiasi gani, hatuwezi kumaliza yote tunayotaka kufanya.

Kitabu kinatupa mtazamo tofauti wa kuuangalia muda na kupangilia namna bora ya kuutumia ili maisha yetu yawe bora.
Tuweze kupata utulivu wa kutosha huku pia tukikamilisha yale ambayo ni muhimu.

Karibu tujifunze dhana hii ya tofauti kwenye usimamizi na matumizi ya muda wetu ili tuweze kufanya makubwa na kufanikiwa pia.

Uchambuzi kamili wa kitabu hiki, pamoja na kitabu chenyewe vinapatikana kwenye channel ya Telegram ya SOMA VITABU TANZANIA.
Jiunge sasa na channel hiyi kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania upate chambuzi za vitabu na vitabu vyenyewe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.