2537; Fursa mchepuko.

Nimewahi kuandika kwamba hofu ni lile unachokiona pale unapoondoa umakini wako kwenye ndoto zako kubwa.

Leo nakwenda kuongezea hilo kwamba unaziona fursa mchepuko pale unapoondoa umakini wako kwenye ndoto zako kubwa.

Fursa mchepuko ni zile fursa zinazoonekana kuwa nzuri na zenye manufaa sana kwako, lakini ili uzifanyie kazi inabidi uache kile unachofanya sasa.

Ni fursa mchepuko kwa sababu zinakutoa kwenye ndoto zako kubwa na malengo yako makuu na kukuhangaisha na mambo mengine.

Fursa hizo mchepuko huwa huzioni unapoanza kitu, kwa sababu wakati huo unakuwa na hamasa ya hali ya juu, huoni kingine chochote.

Lakini kadiri unavyokwenda na kuzoea, huku ukikutana na changamoto mbalimbali, umakini wako unaanza kuhama kutoka kwenye ndoto zako kubwa na unaanza kuangalia mambo mengine.

Hapo ndipo inakuwa rahisi wewe kushawishika na fursa za pembeni, kuona zina matokeo ya haraka.

Lakini ukweli ni hakuna kitu cha thamani chenye matokeo ya haraka. Ni hadaa tu ambayo inataka kukutoa kwenye yale ya msingi kwako.

Kwani hata ukikubali kufanyia kazi fursa hiyo mchepuko, haitachukua muda mrefu utaona fursa nyingine nzuri zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Jua kwa hakika ndoto zako kubwa na weka malengo ya kuzifikia. Chagua fursa kuu utakayofanyia kazi kufikia ndoto hizo. Kisha funga macho yako kwenye fursa nyingine zozote. Hata zije kwako kwa ushawishi mzuri na rahisi kiasi gani, usihangaike nazo, jua hizo zinakuja kwa lengo la kukuondoa kwenye ndoto yako kuu.
Weka unakini wako wote kwenye ndoto yako kuu na usikubali kuyumbishwa na chochote.

Tafakari;
Jambo lolote lenye thamani na manufaa makubwa, huwa linahitaji muda na juhudi kubwa kulijenga. Huwezi kufanya hivyo kama kila wakati utakuwa unahangaika na fursa mpya. Chagua kuwa kipofu kwenye fursa mpya nyingi zinazokuja kwako ili upate nafasi ya kuweka kazi ya kutosha kwenye fursa yako kuu.

Kocha.