2541; Unakopotezea nguvu zako.
Waangalie watoto wadogo, huwa hawawezi kutulia sehemu moja kwa muda mrefu.
Waweke watoto mahali na baada ya muda mfupi utawakuta wakirukaruka na kukimbizana.
Hiyo ni kwa sababu ndani yao kuna nguvu kubwa inayochemka na inayotafuta mahali pa kutokea.
Hiyo ndiyo inayowasukuma wafanye yale wanayofanya.
Nguvu hiyo huwa haiwezi kutulia yenyewe, na kwa kuwa watoto wadogo huwa hawana aibu wala kujali wengine wanawachukuliaje, huruhusu nguvu hiyo itoke.
Sisi watu wazima pia tuna nguvu kama hizo walizo ndani yetu.
Lakini kwa kuwa sisi tuna aibu na tunajali sana wengine wanatuchukuliaje, tunatumia nguvu kubwa kutuliza nguvu hiyo ya ndani.
Kwa hiyo tunachofanya ni kupoteza nguvu kwenye kuzuia nguvu ya ndani.
Yaani una nguvu kubwa ndani yako inayotaka kufanya vitu, lakini wewe unatumia nguvu kubwa zaidi kutuliza nguvu hiyo.
Ndiyo maana unajikuta tayari umeshachoka kabla hata hujaanza kufanya kitu chochote.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapopata msukumo wa kufanya kitu ambacho ni sahihi, utashawishika kujizuia usifanye. Hapo jua unakubali kupoteza nguvu zako.
Ondokana kabisa na hiyo hali, nenda na msukumo wako wa ndani kwenye kufanya yale ambayo ni sahihi na utaweza kufanya makubwa sana.
Tafakari;
Usipoteze nguvu zako kuzuia nguvu kubwa ya ndani inayotaka ufanye vitu. Peleka nguvu zako kwenye kufanya vitu sahihi na vinavyoonekana, hivyo ndiyo vitakavyoleta mabadiliko.
Kocha.