2549; Taarifa ya upande mmoja.
Pale ambapo kuna jambo linalohusisha pande mbili, kamwe usikubali taarifa ya upande mmoja pekee.
Hata kama inashawishi na kuaminika kiasi gani, taarifa yoyote ile haijakamilika kama haina pande zote zinazohusika.
Sisi binadamu huwa ni rahisi kuona makosa ya wengine lakini ni wagumu sana kuona makosa yetu wenyewe.
Ndiyo maana ya ile kauli inayosema nyani haoni matako yake.
Wanapokosea wengine huwa tunaona wamefanya kwa makusudi.
Tunapokosea sisi huwa tunaona ni bahati mbaya.
Na huwa tunafanya hivyo siyo kwa makusudi, bali ni sehemu ya udhaifu wetu.
Hivyo kuepuka udhaifu huo usipelekee ufanye maamuzi mabovu, penda kusikiliza pande zote zinazohusika kabla ya kufikia maamuzi.
Tena ikiwezekana sikiliza kila upande kwa wakati wake na kisha sikiliza pande zote kwa pamoja.
Utajifunza mengi na hata wao wanajifunza mengi kutoka kwa wenzao.
Sehemu kubwa ya changamoto za kwenye maisha ni matokeo ya mawasiliano ambayo hayajakamilika. Mtu kutokuelewa vizuri kitu fulani au kukielewa vibaya.
Pale mawasiliano yanaponyooka, changamoto zinapungua.
Hatua za kuchukua;
Mtu anapokuja kwako na kueleza jambo lake na mtu au watu wengine, sikiliza kwa makini bila kuhukumu au kufikia maamuzi yoyote.
Baada ya hapo tafuta nafasi ya kusikiliza tena na upande wa pili kwa makini bila kuhukumu au kuamua.
Ni baada ya kusikiliza pande zote mbili ndiyo unaweza kuona jinsi kila upande umechangia kufikia pale walipofikia.
Tafakari;
Hakuna changamoto au hali ya kutokuelewana kwa pande mbili inayotengenezwa na upande mmoja tu. Ni lazima pande mbili au zaidi zihusike. Kama unataka kutatua hali ya aina hiyo, hakikisha umesikiliza pande zote zinazohusika.
Kocha.