2553; Mubashara na marudio.
Ukiangalia mchezo wowote ule mubashara, kwa wakati ambapo unaendelea, unakuwa hujui nini hasa kitatokea muda wowote ujao.
Hivyo unaangalia kwa shauku kubwa, ukijua chochote kinaweza kutokea.
Ukiangalia mchezo huo huo kwa marudio, unakuwa huna shauku kubwa, kwa sababu tayari unajua nini kitakwenda kutokea. Kama ni magoli yatafungwa, unajua kabisa ni kwenye dakika zipi magoli hayo yanafungwa.
Utajua sehemu nyingi za mchezo huo ni za kawaida sana na sehemu chache ndiyo zenye matukio ya kusisimua.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo, wakati unayaishi huwezi kujua nini kitatokea mbele. Lakini baadaye unapokuja kuangalia nyuma ndiyo unaona baadhi ya matukio yalivyokuwa na umuhimu na yameleta mabadiliko makubwa.
Usikubali kuyaishi maisha yako kwa mazoea kama vile unaangalia mchezo wa marudio.
Badala yake yaishi kwa shauku kama vile unaangalia mchezo ambao ni mubashara.
Chukulia kila unachopitia kwa umakini mkubwa, ukijua kinaweza kuleta matokeo makubwa na yatakayobadili kabisa maisha yako.
Baadaye utakapokuja kuangalia nyuma ndiyo utaelewa jinsi maisha yako yalivyoweza kubadilika.
Hatua ya kuchukua;
Ishi mubashara na sio kwa marudio. Ishi kwenye wakati uliopo kwa kuweka umakini wako kwenye kila kinachotokea, maana ndiyo njia ya kuweza kutumia vyema kila unachopitia.
Kila unalopitia lina fursa ya kuyabadili maisha yako, kama utalitumia vizuri.
Tafakari;
Unapokuwa hujui nini kinakwenda kutokea, unakuwa na shauku na umakini mkubwa.
Unapokuwa na uhakika wa kinachokwenda kutokea unaenda kwa mazoea.
Mara zote kuwa kwenye hali ya kutokuwa na uhakika wa kinachokwenda kutokea, ndiyo njia ya kuweza kufanya makubwa.
Kocha.
Asante Sana kocha, nachagua kuishi mubashara
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike