#SheriaYaLeo (57/366); Toka nje ya mazoea yako.
Kadiri unavyoendelea kujifunza kwa kufanya, utajikuta umejijengea aina fulani ya mazoea ambayo ndiyo unaridhika nayo.
Mazoea hayo yanakuwa yametokana na wale ambao unakuwa umejifunza kutoka kwao, maana nao pia wanakuwa wamefikia kilele fulani na kufanya zaidi kwa mazoea.
Huwezi kufikia ubobezi wa hali ya juu kama utaendelea kubaki kwenye mazoea hayo.
Unapaswa kutoka nje ya mazoea hayo mara kwa mara kwa kujifunza na kujaribu vitu vipya.
Hilo litakupa hofu maana utajiona hujawa tayari, utaona ni kwenda kinyume na wale waliobobea ambao unajifunza kwao.
Lakini hiyo ni hatua muhimu sana kwako kuchukua maana inavunja mazoea uliyojijengea na kukuweka kwenye fursa ya kufanya mapya na makubwa zaidi.
Unapochukua hatua hii ya kutoka nje ya mazoea yako usiogope kukosea au kukosolewa, jua hayo yote ni sehemu ya kujifunza ili uweze kufikia ubobezi wa juu kabisa.
Ubobezi wako utatokana na upekee wako. Pamoja na kujifunza kwa wengine, hutaweza kubobea kwa kuendelea na yale uliyojifunza kwao.
Bali utabobea kwa kufanya vitu kwa namna ya kipekee kabisa kwako.
Na hilo litawezekana kama utakuwa mtu wa kujifunza na kujaribu vitu vipya, kutoka nje ya mazoea.
Sheria ya leo; Kila mara jifunze na kujaribu vitu vipya hata kama unajiona hujawa tayari. Kutoka nje ya mazoea ndiyo njia ya kufikia ubobezi wa hali ya juu kabisa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu