#SheriaYaLeo (64/366); Mchakato wa ubunifu.

Hakuna darasa la ubunifu, yaani ubunifu ni kitu ambacho huwezi kufundishwa na mtu yeyote yule.
Ubunifu ni kitu ambacho unajijengea wewe mwenyewe kwenye kile unachokuwa unafanya.

Kupitia wale waliobobea kwenye maeneo mbalimbali, tunajifunza hatua muhimu za kujijengea ubunifu kwenye kile unachofanya.

Hatua ya kwanza ni kuwa muwazi mwanzoni. Hapa unapaswa kuepuka kujifungia kwenye kitu kimoja au mtazamo wa aina fulani lekee. Unapaswa kuwa wazi katika kujifunza, kufikiri na mtazamo wako kwenye mambo mbalimbali. Kwa njia hii utaweza kujua na kupitia mengi.

Hatua ya pili ni kuwa na uelewa mpana sana wa lile eneo ulilochagua kufanyia kazi na maeneo mengine yanayoendana na eneo hilo. Kadiri unavyojua zaidi ndivyo akili yako inavyoweza kujenga muunganiko mwingi unaoleta ubunifu.

Hatua ya tatu ni kutokuruhusu mazoea kuingia kwenye kile unachofanya. Usifanye kitu chochote kwa mazoea, badala yake kila wakati jisukume kuwa mpya na bora zaidi. Popote ulipofika na matokeo yoyote unayopata, jua unaweza kwenda zaidi ya hapo. Usiridhike na popote ulipofika, usijipe uhakika kwenye jambo lolote. Kila mara jisukume zaidi na hilo litafanya uje na ubunifu mpya kila mara.

Hatua ya nne ni kuwa mvumilivu na kujipa muda kwenye kile unachofanya. Ubunifu ni kitu ambacho hakiwezi kulazimishwa kitokee kwenye wakati fulani. Bali ni kitu ambacho huwa kinatokea chenyewe wakati unapokuwa sahihi. Hivyo unapaswa kuwa mvumilivu na kujipa muda kwenye kile unachofanya, kuendelea kuweka mchakato na kujua matokeo yatakuja kwa wakati wake.

Jijengee mchakato wako wa ubunifu kwenye kile ulichochagua ili uweze kufanya makubwa na kubobea zaidi.

Sheria ya leo; Ufanye muda kuwa rafiki yako wa karibu kwenye safari ya ubobezi. Miaka mingi ijayo utakapoangalia nyuma, utaona jinsi muda ulivyokuwezesha kufikia ubobezi kwa kukaa kwenye mchakato wa ubunifu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu