#SheriaYaLeo (65/366); Angalia kwa upana na fikiri mbele zaidi.

Kwenye mazingira yoyote yenye ushindani, ambapo kuna washindi na washindwa, yule mwenye mtazamo mpana na anayefikiria kwa ukubwa zaidi ndiye anayeshinda.

Na sababu ni rahisi, mtu huyo anakuwa na uwezo wa kufikiri zaidi ya pale alipo kwa wakati huo na kuweza kudhibiti hali nzima kupitia mkakati mpana.

Watu wengi wana mtazamo mdogo na kufikiri kwa udogo mno, tena kwa mambo yaliyo mbele yao tu.
Maamuzi yao yanaathiriwa sana na kile wanachopitia, ni rahisi kutawaliwa na hisia na kuweka uzito mkubwa kwenye kitu kuliko kinavyostahili.

Ili kufika kwenye ubobezi, lazima uwe na mtazamo mpana na ufikiri mbele zaidi. Lazima ujifunze namna ya kuendelea kukuza mtazamo wako.
Unafanya hivyo kwa kujua kusudi kubwa la maisha yako na jinsi kila unachofanya kinagusa kusudi hilo na manufaa yake kwa walio wengi.

Kwa kila unachofanya, angalia ni kwa namna gani kinaungana na picha kubwa uliyonayo.
Angalia kwa upana na fikiri mbele zaidi inapaswa kuwa kauli mbiu yako kwenye safari yako ya ubobezi.

Sheria ya leo; Mtu mwenye mtazamo mpana zaidi ndiye anayeshinda. Panua mtazamo wako na fikiri mbele zaidi ili uweze kufika na kudumu kwenye ubobezi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu