2564; Aina tatu za urafiki.

Ya kwanza ni urafiki wa faida.
Huu ni wa nipe nikupe. Unakuwa na urafiki na mtu kwa sababu kuna kitu unataka kutoka kwake. Pale uhitaji unapoisha, urafiki nao unakufa.
Huu ni urafiki dhaifu kabisa na ambao huwa haudumu.

Ya pili ni urafiki wa raha.
Au kwa maneno mengine, urafiki wa ‘kula bata’. Huu ni urafiki wa kukutana pamoja wakati wa raha na starehe mbalimbali. Hapa ni marafiki ambao mnakunywa pamoja au kusafiri pamoja n.k.
Urafiki huu pia siyo imara sana kwani mtu anaposhindwa kushiriki hizo starehe, urafiki unakufa.

Ya tatu ni urafiki wa tabia.
Huu ni urafiki wa kumkubali mtu kutokana na kile kilicho ndani yake, ambacho kinaendana sana na wewe.
Tofauti ya urafiki huu na wa aina nyingine ni watu kujuana kwa ndani na kusaidiana kuwa bora zaidi.
Marafiki wa tabia wanajuana uimara na udhaifu wa kila mmoja, wanajua malengo ya kila mmoja na kuweza kusaidiana kupiga hatua zaidi.
Urafiki huu unahitaji kazi na hivyo mtu hawezi kuwa na marafiki wengi wa aina hii.
Ila uzuri ni urafiki ambao unaweza kudumu kwa muda mrefu na ukawa na manufaa kwa kila mmoja.

Hatua ya kuchukua;
Tathmini marafiki wote ulionao na wagawe kwenye aina hizo tatu. Angalia ni marafiki wangapi wa tabia unao. Weka nguvu zako nyingi kwenye kujenga zaidi marafiki wa tabia ili kila mmoja aweze kunufaika kwa kusukumwa kuwa bora zaidi.

Tafakari;
Kadiri urafiki ulivyo rahisi kujenga na kuendesha, ndiyo unavyokuwa wa juu juu, usio na manufaa makubwa na usiodumu kwa muda mrefu.
Kama unataka urafiki uwe bora, lazima uweke kazi ya kutosha katika kuujenga, kuukuza na kuuendeleza.

Kocha.